BAADA ya mawakala wa TP Mazembe kutua nchini Tanzania wiki hii kwa ajili ya kunasa baadhi ya saini za wachezaji mbalimbali, imebainika kuwa wameamua kumuungia mchezaji Ibrahim Ajibu Migomba ambaye walikuwa wakimtaka awali bila mafanikio.
Awali, TP Mazembe ya DR Congo ilikuwa ikimuhitaji mchezaji huyo ambaye walikuwa wakifanya mazungumzo kupitia simu lakini mwisho dili hilo halikufanikiwa kwani aliendelea kuitumikia timu yake ya Yanga.
Moja ya mawakala wa TP Mazembe ambaye yupo Tanzania, Patrick Mazembe alisema kuwa mawakala waliokuja nchini wapo kwa ajili ya kunasa baadhi ya wachezaji wachezaji akiwemo Ajibu jambo ambalo wanaamini watampata kama watafanikiwa kuonana na kuzungumza naye.
“Kuna wachezaji Mazembe imewaona huko Tanzania na ndiyo maana mawakala wengi wanakuja huko kujaribu kuwashawishi baadhi ya wachezaji wa huko akiwemo Ibrahim Ajibu Migomba,” alisema.
Pia alielezea kuwa dili la kwanza na Ajibu lilishindikana kwa kuwa uongozi wa Mazembe ulikuwa ukiwasiliana na Ajibu kupitia simu yake ya mkononi jambo ambalo lilisababisha Ajibu kuwazimia simu baada ya kuona maslahi ni madogo.
“Awali, uongozi wa Mazembe ulikuwa ukiwasiliana na Ajibu kupitia simu jambo ambalo liliwagharimu kwani aliamua kuizima simu yake baada ya kuona mshahara mdogo ambao Mazembe walimpa, ndiyo maana kwa sasa tumeamua kumfuata Ajibu nchini Tanzania,” alisema wakala huyo.