Rais wa Marekani Donald Trump amesitisha hatua ya kuishambulia Iran muda mfupi baada ya kutoa idhini ya kufanya hivyo kujibu shambulio la Iran lililoidungua na kuiangusha ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani.
Gazeti la New York Times limeripoti likiwanukuu maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Marekani, wakisema kuwa rais trump aliidhinisha kufanywa mashambulizi kwa kuyalenga maeneo kama rada za jeshi na mizinga ya kufytua makombora.
Mashambulizi hayo yalipangwa kufanyika kabla ya mapambazuko ya siku ya leo Ijumaa kujibu shambulio la Iran la kuiangusha ndege ya jeshi la Marekani kwa madai ya kuingia kwenye eneo lake la bahari.
Kulingana na gazeti hilo, afisa mmoja wa utawala wa Trump amesema ndege za kivita zilikuwa angani na meli zilijiweka tayari lakini hakuna kombora lililofyatuliwa wakati amri ya kusitisha mashambulizi hayo ilipotolewa.
Uamuzi huo wa ghafla wa kusitisha kuishambulia Iran umezuia kile ambacho kingekuwa hatua ya tatu ya kijeshi ya utawala wa Trump katika eneo la mashariki ya kati baada ya kuvishambulia vituo vya jeshi la Syria mwaka 2017 na 2018.
Hatahivyo haijafahamika mara moja iwapo mashambulizi dhidi ya Iran yataendelea na haijawa wazi uamuzi huo wa Trump wa kuyasitisha umechochewa na kitu gani.
Hapo jana rais Trump alisema Iran imetenda kosa kubwa kwa kuiangusha ndege ya Marekani katika anga ya mlango bahari wa Hormuz.
Rais Trump alipooulizwa kuhusu hatua atakazochukua alisema kwa mkato "mtafahamu hivi karibuni".
Lakini pia Trump aliashiria kuwa huenda shambulio hilo huenda lilifanywa kimakosa na mtu aliyepewa maelekezo na mamlaka za Iran.
Iran yalalamika kwa Umoja wa Mataifa
Wakati huo huo Iran imesema imeyapata mabaki ya ndege isiyo na rubani ya jeshi la Marekani katika eneo lake la bahari baada ya kuidungua
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Mohamed Javed Zarif amesema kupitia ukurasa wa Twitter kuwa ndege hiyo ilidunguliwa baada ya kukiuka utaratibu na kuingia kwenye anga la Iran.
Katika barua kwenda Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwa Katibu mkuu wa Umoja huo, Iran imelalamika dhidi ya kile ilichoita kuwa vitendo hatari na vya uchokozi vya jeshi la Marekani kwenye eneo lake la bahari.
Marekani kwa upande wake imesema ndege iliyoangushwa ilikuwa kwenye eneo la maji ya kimataifa.
Katika hatua nyingine viongozi wa bunge la Marekani wametoa wito wa kuchukuliwa tahadhari kuepusha kuongezeka mvutano na baadhi ya wabunge wamesisitiza kuwa Ikulu ya Marekani inapaswa kuliarifu bunge na kupata idhini yake kabla ya kuchukua hatua ya yoyote dhidi ya Iran