Serikali imeeleza kuwa inatarajia kuja na utaratibu mpya wa kutibu ugonjwa wa Dengue ambao umezuka katika baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Dar es Salaam na kupelekea vifo kwa baadhi ya watu na wengine kuugua.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Ummy Mwalimu wakati akijibu swali la Mbunge wa Ilala Mussa Zungu ambaye alihoji juu ya Serikali kugawa dawa mpya zitakazomaliza mbu wa ugonjwa wa Dengue.
Akiuliza swali hilo Bungeni, Mbunge Zungu amesema kuwa, "bado kuna changamoto kwenye upambanaji wa Dengue, Serikali itabadilisha dawa zinazotumika ili wananchi washiriki wazimwage kwenye maeneo yao, Mheshimiwa Naibu Spika ni kwamba sasa hivi Mbu wa Dengue wameanza kuingia kwenye daladala".
Akijibu swali hilo Bungeni, Waziri Ummy amesema "suala hili limeanza kufanyiwa kazi na Serikali, ndani ya siku 2 tutatoa kauli rasmi jinsi gani tumechukua hatua za kupambana na Dengue".
"Niwaambie pia wananchi hakuna njia nyingine ya kujikinga na ugonjwa Dengue zaidi ya kuwatokomeza mbu hao," ameongeza.