UCHOKOZI WA EDO: Nongwa za akina Bashe zinasaidia chama


By Edo Kumwembe
Nimemsikia Katibu Mwenezi akisema wabunge wa chama chake ambao wana nongwa majina yao hayatarudi mwaka 2020. Nikacheka sana. Hawa wenye nongwa ni akina Hussein Bashe. Wanajulikana tu hata wasipotajwa majina.

Hawa ni wale wabunge wa Chama Tawala ambao wameruhusu kutumia akili zao hadharani. Kuna wabunge wengi wa chama tawala ambao wana akili nyingi ukikaa nao katika meza za baa, lakini wakiingia mjengoni wanagoma kutumia akili zao, kisa? Hofu.

Binafsi nadhani hawa akina Bashe ndio ambao wanakiweka chama tawala hai. Bunge la vyama vingi lilipoingia wabunge wa upinzani walipata umaarufu mkubwa. Sio kwa sababu wana akili sana, hapana, kwa kuwa maarifa yao wanayaweka hadharani. Wale wabunge wa chama tawala akili zao wanatuletea katika vikao vya baa.

Unapowapata watu kama akina Bashe upande wako, unapata fursa ya kujitetea na kujigamba hadharani “hata sisi tunao watu kama akina Zitto Kabwe, msitutishe nyie wapinzani.” Unapoamini Bashe ana nongwa au anaiweka Serikali katika wakati mgumu ni vizuri kuangalia na huu upande mwingine. Mwanao anaweza kuwa mkorofi lakini kama ameamua kuwa bondia basi haina shida.

Inapofikia suala la kila mbunge wa chama tawala awe anaongea kama yule mbunge fulani wa Dodoma, chama kinateketea. Katika chama unahitaji wapiga domo na unahitaji wajenga hoja wazuri wenye uwezo wa kutafakari mambo na kuongea kama wapinzani kwa ajili ya kushusha umaarufu wa wapinzani.

Hata ikitokea mbunge huyu akawakosoa wapinzani anakuwa na uwezo wa kujenga hoja ambazo wananchi watamuelewa kwa nini upinzani ni mbovu na haufai. Lakini kuna mwingine akiongea kuhusu ubovu wa wapinzani hawezi kueleweka kwa sababu siku zote hajawahi kuongea kitu cha maana zaidi ya mipasho. Kuna wengine wanasikilizika. Inasikitisha pale mheshimiwa mwenezi anaposema “wana nongwa”.

Wabunge kama hawa inabidi watunzwe na watumike katika kuzitangulia akili za wapinzani. Wakati wapinzani wakijulikana wanataka kusema hiki, wao wanatangulia kusema, baadae hata wapinzani wakisimama wanaonekana wanarudia tu. Ni muhimu kuwa na watu hawa. Unapoamini wana nongwa unajiharibu mwenyewe. Unawafanya akina Zitto waonekane wanaongea vitu vipya kumbe akina Bashe wanavijua kwa muda mrefu tu.


Mwananchi
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad