Ugonjwa wa Kipindupindu Wazidi Kusambaa Dar Watatu Wafariki na Waliolazwa Wafikia 55

Ugonjwa wa Kipindupindu waendelea kusambaa kwa kasi Dar es salaam. Taaifa zinasema mpaka Jumapili hii watu watatu wamefariki dunia baada ya kuibuka kwa kipindupindu katika Jiji la Dar es Salaam wiki moja iliyopita.



Hadi  Jumapili ya jana, wagonjwa waliolazwa kwenye kambi tatu tofauti za wagonjwa wa kipindupindu walikuwa 55.

Hayo yamesemwa leo Jumapili Juni 2, 2019 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ziara yake aliyoifanya Bonde la Jangwani jijini hapa.

Waziri Ummy amesema vifo viwili vimeongezeka kutokea Temeke ambako wagonjwa wengine 34 wamegundulika wilayani humo.

“Jumla ya vifo sasa ni vitatu, kwa Wilaya ya Temeke peke yake ni viwili na Ilala kimoja, Temeke pia ina wagonjwa 34, Ilala 19 na Kinondoni wagonjwa wawili,” amesema waziri huyo.

Ameyataja baadhi ya maeneo korofi kwa ugonjwa huo ni  Keko, Tandika, Buza, Kariakoo, Vingunguti, Mchikichini na Kivule.

Waziri Ummy amesema ugonjwa huo hutokana na maambukizi katika utumbo mdogo wa binadamu uletwao na vimelea vya bakteria vijulikanavyo kitaalamu kama ‘Vibrio cholerae’.

Amesema vimelea hao hupendelea kuishi katika kinyesi cha binadamu,  “mtu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kunywa maji ama chakula kilichochafuliwa na kinyesi.”

Aidha, amesema mtu anaweza kuepuka ugonjwa huo kwa kunywa maji safi na salama na kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa vyema.

“Ni muhimu kunawa mikono baada ya kutoka chooni na kabla ya kula chakula, tunashauriwa kufunika chakula kikiwa mezani ili nzi wasitue juu yake na kujenga choo umbali wa angalau mita 30 kutoka chanzo cha maji.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad