Usajili Mpya Simba Hatari Tupu

SIMBA imesisitiza kwamba watafanya usajili wa aina yake msimu huu lakini wachezaji wawili watakaowasajili ni mshtuko.



Kikosi hicho kilichopo chini ya muwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo’ kimetwaa ubingwa mara mbili mfululizo na sasa kinajiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza mwezi Agosti.



Katika usajili wao mpya, Simba wametamka kwamba hawataleta mchezaji yeyote kwa majaribio kwani wao wameshavuka levo hiyo. Haji Manara ambaye ni Ofisa Habari wa Simba amesema kwamba;

“Hatufanyi masihara kwenye suala la usajili, siyo kila siku mara huyu mara yule, sisi hatufanyi usajili wa kujaribu.”



“Timu inakwenda kucheza Ligi ya Mabingwa unakwenda kumchukua mchezaji aje kwenye majaribio? Sasa hivi ni kusajili tu.

“Tutashusha usajili wa uhakika ambao kila mtu atashtuka na kusema kweli Simba imejiandaa kwenda kuchukua Kombe la Afrika.

“Kila mtu atashtuka, sisi levo yetu si ya kushindana na Yanga sisi tunafanya mausajili makubwa, tutaleta watu kwelikweli.

“Tutasajili wawili nao ni mshtuko kwelikweli, hatufanyi masihara kweli suala la usajili, tunataka kuifikisha nchi yetu kwenye sehemu ambayo kila mtu ataiheshimu,” alisisitiza Manara.



Ibrahim Ajibu aliyemaliza mkataba wake na Yanga ni miongoni mwa wachezaji wazawa wanaohusishwa na Simba mpya inayoingia kwenye Ligi ya Mabingwa Agosti mwaka huu.



Mo alisisitiza hivi karibuni kwamba atasajili wachezaji wa maana na bajeti itakuwa ni zaidi ya ile ya mwaka jana ambayo iliifikisha Simba kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.



Msimu ujao Tanzania itaingiza timu nne kimataifa ambazo ni Simba na Yanga Ligi ya Mabingwa na Azam na KMC Kombe la Shirikisho. Hii ni mara ya kwanza kutokea kwa nchi ya Afrika Mashariki kuingiza timu nne kwenye mashindano ya Caf.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad