Rais wa shirikisho la soka duniani Gianni Infantino anakabiliwa na upinzani mkali, kutoka kwa mmoja wa makamu wake juu ya mpango wa kumteua katibu mkuu Fatma Samoura, kwenye majukumu ya ziada ya kulichunguza shirikisho la soka la afrika CAF.
Aleksander Ceferin ambaye ni mkuu wa shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, alikuwa miongoni mwa makamu wa rais wa FIFA walioombwa na Infantino siku ya Alhamis, kuidhinisha uteuzi wa Samoura atakayeongoza ujumbe wa FIFA katika kipindi cha miezi sita kuanzia mwezi Agosti.
Samoura anapigiwa upatu kuongoza ujumbe utakaofanya ukaguzi wa kifedha katika shirikisho la soka barani Afrika CAF.
Hatua hiyo inakuja, mnamo wakati rais wa CAF Ahmad akikabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha. Infantino ametoa mapendekezo hayo katika barua iliyosambazwa kwa baraza la FIFA linalojumuisha viongozi wa kikanda wanaohudumu kama makamu wa rais katika shirikisho hilo.