Wabunge KENYA Watofautiana Kuhusu Matamshi ya Jaguar



Wabunge wa bunge la Jamhuri ya Kenya, wametofautiana kuhusu matamshi ya mbunge wa jimbo la Starehe lililopo jijini Nairobi nchini humo, Charles Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar kuhusu kuwatishia raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo.

Matamshi hayo yaliwasilishwa mbele ya kikao cha bunge ili kujadiliwa na kuweza kuchukua hatua stahiki kuhusu mbunge huyo kuwatishia raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanaoishi na kufanya kazi nchini humo.

Aidha, hatua hiyo imejiri huku Mbunge huyo akiwa mikononi mwa Polisi ambapo anasubiri kufikishwa mahakamani.

Kulingana na mtandao wa kituo cha kurushia matangazo cha Televisheni ya Citizen nchini humo, kimesema kuwa licha ya wabunge wengi kushutumu jinsi ambavyo Jaguar alitoa hoja yake , baadhi yao walikubaliana kwamba kuna utata mkubwa kuhusiana na raia wa kigeni wanaoishi nchini humo.

Suala hilo liliwasilishwa katika bunge la nchi hiyo na mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Uhusiano wa kigeni, Katoo Ole Metito katika taarifa yake, akithibitisha kwamba raia wa kigeni hususani kutoka Jumuiya ya Afrika mashariki wana uhuru wa kufanya biashara nchini Kenya.


”Tunalaani vikali matamshi yoyote ya chuki yanayokiuka msimamo huu unaotuleta sisi pamoja kama taifa na kuthibitisha sera ya kuwakaribisha raia wote wa kigeni”, amesema mbunge huyo wa Kajiado kusini.

Hivi karibuni mbunge huyo wa jimbo la starehe alitoa matamshi ambayo yaliashiria kuwabagua raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo kwa kuwatuhumu kuchukua nafasi za Wakenya.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad