Wafanyabiashara Mkoani Iringa wameandamana kwenda kwa Mkuu wa Wilaya wakilalamikia Askari wa Jeshi la Polisi Mkoani humo kuwapiga na kuwadhalilisha nyakati za usiku kwa kisingizio cha kuongeza muda wa kufunga maeneo ya biashara zao jambo ambalo sio la kweli.
Wafanyabiashara hao wanaomiliki biashara za vinywaji waliandamana jana Juni 13, kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richadi Kasesela kupeleka kilio chao hicho ambacho kimedumu ndani ya wiki tatu mpaka sasa.
Akizungumza kwenye kikao hicho mmoja wa wafanyabiashara hao, Happy Matanji alisema askari hao wa doria wanaokuja usiku kuwalazimisha kufunga biashara zao kabla ya wakati na wamekuwa wakiwadhalilisha na kuwapiga wateja wao bila sababu za msingi.
"Hawa Askari wanatunyanyasa sana hasa huyu askari anayeitwa Wambura amekuwa akija kwenye bar zetu anawakalisha wateja chini anaenda nje anakata fimbo na wengine wanatembea na waya za umeme wanawapiga nazo watu migongoni na miguuni hadi watu wengine wanashindwa kutembea’’ alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Richard Kasesele amekiri kuwa askari waliofanya vitendo hivyo wamekosea na kuwaombea msamaha kwa wafanyabiashara hao ambapo alisema kuwa Askari hao walikuwa wakitumia nguvu kupita kiasina kwamba hawakupaswa kuwanyanyasa na kuwatesa watu kiasi hicho kwani vitu vingine ni kuelekezana na sio kutumia nguvu.
"Mimi niwaombe wafanyabiashara hawa wawe wapole serikali yao imesikia kilio cha na wote waliofanya hivyo hawatabaki salama na kuanzia sasa hizo bar zenu fungeni saa saba halafu nione mtu atakayekuja kuwagusa nitakufa naye nawambia,” alisema.
Wafanyabiashara wa Bar Waandamanaji Wakilalamikia Polisi
0
June 15, 2019
Tags