Karibu watu 100 wameripotiwa kuuawa katika kijiji cha watu wa jamii ya Dogon nchini Mali.
Shambulio hilo limefanyika katika kijiji cha Sobale Kou, karibu na mji wa Sanga, kwa mujibu wa kituo cha habari cha Ufaransa RFI.
Miili ya waliouawa imeteketezwa moto, anasema afisa katika eno hilo na kuongeza kuwa shughuli ya kutafuta miili zaidi inaendelea.
Kumeshuhudiwa visa kadhaa vya mashambulio nchini Mali katika miezi ya hivi karibuni na baadhi ya mashambulio hayo yanasadikiwa kutekelezwa na makundi ya kijihadi.
Mzozo kati ya wawindaji wa jamii ya Dogon na wafugaji wa jamii ya Fulani umekuwa ukiibuka mara kwa mara.
Meya wa mji wa jiji la Bankass, Moulaye Guindo, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wa jamii ya Fulani kutoka wilaya hiyo walishammbulia Sobane-Kou after giza likiingia.
Afisa wa eneo la Koundou, ambalo linajumuisha kijiji kilichoshambuliwa, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa: " sasa hivi tunathibitisha vifo vya watu 95. Miili imechomwa na bado tunaendelea kutafuta maiti zingine."
Mapigano kati ya jamii hizo mbili imeongezeka tangu wanamgambo wa kiislam walipovamia eneo la kaskazini mwa Mali mwaka 2012.
Mwezi machi mwaka huu zaidi ya wanavijiji 130 wa jamii ya Fulani waliuawa na watu waliyokuwa wamejihami na amabo walidaiwa kuvalia mavazi ya kitamaduni ya wawindaji wa Dogon.
Tofauti kati ya jamii ya Fulani na Dogon ilisuluhishwa kupitia mashauriano ya amani lakini ghasia zilizosambaa maeneo ya kati ya Mali mwaka 2015 -ziliathiri udhibiti wa serikali hali iliyosababisha kuingizwa kwa silaha.
Pande zote mbili zinalaumiana kwa uchokozi na kuanzisha mapigano.