WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka waislamu kote nchini waendeleze utulivu, amani na uadilifu waliouonesha katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwani kwa kufanya hivyo, watasaidia kukuza umoja wa kitaifa, uchumi na kuboresha huduma za jamii.
Amesema ni vema wakatambua kwamba uadilifu waliouonesha ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni silaha muhimu hususan katika kuimarisha maendeleo na kudumisha haki, umoja, usawa, upendo na utulivu.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano, Juni 5, 2019)kwenye Baraza la Eid El Fitri, lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Tanga Beach Resort jijini Tanga.“Nawashi sana kuyaenzi mema yote mliyoyafanya kipindi cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan’’.
Kadhalika, Waziri Mkuu amezipongeza taasisi za Kiislamu na imani nyingine ambazo zimejenga shule ili kuchangia maendeleo ya elimu kitaifa lakini amesisitiza kuwa bado kuna haja ya kuongeza shule nyingine na vyuo zaidi pamoja na kuziboresha zile zilizopo ili kusaidia jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za jamii nchini
Amesema licha ya juhudi inazozichukua, Serikali peke yake haina uwezo wa kueneza huduma za jamii kama vile elimu, afya na maji katika kila pembe ya nchi hivyo, inapotokea taasisi za Kiislamu au madhehebu mengine yakaweka mikakati ya kueneza huduma hizo, basi bila shaka Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo na kuchangia ufanisi wake.
Wakati huo huo, ameitaka BAKWATA ichukue hatua za makusudi katika kuhakikisha huduma nyingi za maendeleo na za kijamii zinaifikia kwenye mikoa mingi zaidi ya pembezoni. “Huu ni wakati muafaka sasa wa kutafakari ni namna gani Watanzania wa maeneo mengine nao watanufaika na uwepo wa huduma mbalimbali kama vile elimu, afya na nyinginezo.“
Kwa upande wake,Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar Zubeir bin Ally ametumia fursa hiyo kuwataka waislam wote nchini wabadilike na waache mazoea ili waweze kusonga mbele kielimu na kiuchumi.
Sheikh Zubeir amesema ni vema kwa waislamu wakajiimarisha kiuchumi kwa sababu kutawaondolea changamoto za kuendesha shughuli zao mbalimbali na hivyo watakuwa wamejiletea maendeleo na kuboresha maisha yao.
Mbali na wito huo pia amewataka waislamu wote wahakikishe wanatii mamlaka yaliyo juu yao , viongozi waliopo madarakani wawe wa kiserikali na wa kidini kama ilivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa [TAKUKURU], Diwani Athuman amesema ili nchi iweze kuendelea kuwa na amani, utulivu na usalama watanzania wote hawana budi kuungana pamoja katika kupiga vita vitendo vya rushwa.
"Rushwa ni dhambi kubwa na hukumu yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni moto kwa sababu rushwa ni kipingamizi kikubwa cha maendeleo, hivyo tuungane pamoja kupinga rushwa ndani ya nchi yetu kama Rais Dkt. John Magufuli anavyotuongoza."
Waziri Mkuu , Kassim Majaliwa Awataka waislamu kote nchini waendeleze utulivu, amani na uadilifu
0
June 06, 2019
Tags