Waziri Mkuu: Tutumie Siku Ya Eid Kwa Kutenda Mema

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amewataka waislamu wote nchini watumie siku kuu ya Eid el Fitr kwa kutenda matendo mema pamoja na kuwakumbuka yatima na wajane.

“Leo ni siku kubwa na muhimu waislamu wanahitimisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea siku kuu ya Eid El Fitr, hivyo tuendeleze matendo mema.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Juni 5, 2019) wakati aliposhiriki swala ya Eid El Fitr katika msikiti wa Anwar uliopo Msasani jinini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema wakati huu ni mzuri kwa kuimarisha mshikamano miongoni mwenu na madhehebu mengine, hivyo hakikisheni mnayaendeleza mambo mema yote.

“Tumeona utulivu uliojitokeza katika mwezi mtukufu, na jambo hili limesisitizwa na viongozi wa dini. Tuendelee kuwa wamoja, tuimarishe mshikamano na tuvumiliane.”

Pia, Waziri Mkuu amewakumbusha wazazi na walezi kuwaongoza watoto kwa kuwapa mafundisho ya dini yatakayowawezesha kumjua Mwenyezi Mungu na kuwa raia wema.

Awali, Imamu wa msikiti huo, Sheikh Mhina alisema waislamu wanatakiwa kuitumia siku ya leo kwa kuhamasisha Amani pamoja na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo.

Pia amewasisitiza wayaendeleze mema yote waliyoyafanya katika kipindi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni pamoja na kuwaheshimu na kuwajali wazazi wao.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad