WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amezitaka taasisi za utafiti wa mifugo nchini kuhakikisha zinafanya tafiti zaidi nchini kwa lengo la kubaini ng’ombe bora wa maziwa ikiwa ni mkakati wa kuongeza upatikanaji wa maziwa nchini.
Ameweka wazi kuwa kwa sasa Tanzania kuna ng’ombe wa maziwa milioni 1,294882 na uzalishaji wa maziwa ni lita bilioni 2.7 kwa mwaka wakati mahitaji ni lita bilioni 11, hivyo kuna upungufu wa maziwa lita bilioni 7.3 kwa mwaka.
Mpina ameeleza hayo wakati wa Maonyesho ya Ng’ombe Bora wa Maziwa nchini Tanzania ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika Viwanja vya Nanenane Mjini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya maziwa kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mifugo.
Akifafanua zaidi kwenye maoesho hayo, Waziri Mpina amesema kuwa Tanzania ni ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo ikiongozwa na Ethiopia kwa Bara la Afrika lakini katika uzalishaji maziwa iko chini ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.
“Kwa mwaka Tanzania kwa upande wa maziwa yanayosindikwa ni lita milioni 70 wakati hapa majirani zetu wa Kenya kwa mwaka wanazalisha maziwa ya kusindikwa lita milioni lita zaidi ya 800.
“Tanzania kwa mwaka tunaagiza maziwa yaliyosindikwa kutoka nje ya nchi lita milioni 20, hivyo serikali inatumia Sh. bilioni 30 kwa ajili ya kuagiza maziwa wakati hapa nyumbani tuna ng’ombe wengi na hii ni aibu ambayo awamu ya tano imeweka mikakati ya kuimaliza,”amesema Mpina.
Amewataka Watanzania na hasa wadau wa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kuchangia fursa hiyo ya uhaba wa maziwa kwa kuzalisha kwa wingi, na kwa upande wa serikali amesema imejipanga vyema kuhakikisha sekta ya mifugo inaleta tija kwa taifa.
“Ukweli uliopo kwa idadi ya mifugo ambayo tunayo hapa nchini, hata hao ambao wanaonekana ni washindani wetu huenda sio washindani kabisa kwetu. Kwa mikakati ambayo wizara yetu inayo na malengo ya serikali ya awamu ya tano, tuna uhakika Tanzania tutakuwa wa kwanza kwa kuzalisha maziwa mengi na yaliyo bora,” amesisitiza.
Kuhusu jumbe ambazo zimetolewa wakati wa maonyesho hayo, amekiri zimezungumzia changamoto ya uhaba wa dawa za chanjo za mifugo na malisho ya mifugo, ambapo amesema serikali imeshaweka mikakati kuondoa changamoto hizo pamoja na nyingine.
Ameongeza kwamba serikali itahakikisha dawa zinapatikana kwa gharama nafuu na si bei ya juu ambayo wafugaji wanauziwa. Pia, ameongeza, wizara imejipanga kukabiliana na magonjwa ya mifugo na kufafanua kupitia maabara za mifugo zilizopo watahakikisha kabla mifugo haijaingia nchini inafanyiwa vipimo kama sehemu ya kukabiliana na magonjwa ya mifugo.
Wakati huohuo, Mpina amesem wizara imedhamiria kuhakikisha bei ya maziwa inaongezeka kwa kuwa bei ya sasa ni ndogo na binafsi anaumia anapoona bei ya lita ya maziwa inakuwa chini ya Sh.1,000.
Akizungumzia ng’ombe bora wa maziwa, amesema kuna idadi kubwa ya ng’ombe hivyo hakuna sababu ya kuagiza mbegu kutoka nje ya nchi na kwamba kupitia tafiti zinazoendelea katika vituo vya utafiti vilivyopo nchini na hasa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania kuna uwezekano wa kuwa na madume mengi zaidi yenye mbegu bora.
“Nikiri yapo malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi kuhusu madume ya ng’ombe aina ya mtamba na tayari wizara na serikali kwa ujumla imeweka mikakati ya kuhakikisha tunakuwa na mitamba mingi zaidi. Hivyo taasisi zetu za utafiti zihakikishe zinafanya tafiti nyingi na katika mikoa mingi zaidi,” amesema.