Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Agustine Mahiga Atoa Ufafanuzi Kuhusu Sheria ya Mirathi

Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Agustine Mahiga amesema kuwa hakuna sheria inayompa mgane haki zaidi ya mjane au kwa namna yoyote kuonesha ubaguzi na kwamba sheria zinaeleza namna mali inavyopaswa kugawiwa kwa wanufaika huku ikiainisha kila mnufaika na kiwango anachopata.

Ametoa kauli hiyo bungeni jana Juni 18, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Silafu Maufi (CCM) aliyetaka kujua ni kwa nini mjane asiandikwe jina lake kwenye hundi na asimame na watoto wake kwa kupewa haki ya kusimamia mirathi.

Akijibu, Dk Mahiga alisema utaratibu unaofanyika unamtaka msimamizi wa mirathi kuwasilisha mchanganuo wa malipo na hundi huandikwa kwa wanufaika wote pasipo kujali jinsia zao.

Alisema pamoja na kuwa na Sheria nzuri, kumekuwa na uelewa mdogo miongoni mwa baadhi ya wananchi kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazohusu utaratibu wa mirathi.

“Wizara yangu kupitia RITA na wadau mbalimbali imekuwa ikitoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu mirathi na itaendelea kubuni mbinu zitakazosaidia ili elimu ya hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi” alisema.

Aliongeza kuwa sheria za nchi zinatambua kuwa mirathi na usimamizi wake unaweza kuongozwa na sheria ya kiislamu au Sheria ya India ya mwaka 1885 kwa wasiokuwa waislamu na kwamba matumizi ya sheria hizo yanaangalia maisha ya marehemu, dini na namna marehemu alivyozikwa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad