Aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Wilaya ya Ilala, Norah Waziri maarufu Nora Mzeru amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na shtaka la kughushi cheti cha ndoa.
Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda amedai leo Ijumaa Julai 12, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi, Anifa Mwingira kuwa Februari 4, 1995 jijini Dar, es Salaam kwa nia ya kudanganya mshtakiwa huyo alighushi cheti cha ndoa chenye usajili namba 00040078.
Amedai kuwa alifanya hivyo kwa nia ya kuonesha kuwa alifunga ndoa na Silvanus Mzeru (marehemu) Februari 4, 1995 katika kanisa Katoliki Mburahati wakati akijua si kweli.
Mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shtaka lake hilo, amekana na kudai Mzeru ni mumewe.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Baada ya kusomewa shtaka hilo mawakili wanaomtetea mshtakiwa, Mtubika Godfrey na Juma Nyamgaruri waliiomba mahakama kumpatia dhamana mteja wao kwa sababu shtaka linalomkabili kwa mujibu wa sheria linadhaminika.
Baada ya kusikiliza hoja hiyo hakimu huyo aliahirisha kesi hiyo namba 365 ya mwaka 2019 hadi Julai 17, 2019 itakapotajwa tena huku mshtakiwa akiachiwa kwa dhamana