BAADA ya juzi Jumatano, Simba kumtangaza Ibrahim Ajibu kuwa mchezaji wao mpya, Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali ameibuka na kufunguka kuwa mshambuliaji huyo alikuwa kama kirusi katika timu yao.
Ajibu ambaye alijiunga na Yanga msimu wa 2017/18 akitokea Simba, msimu uliopita aliisaidia Yanga kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara huku yeye akimaliza kuwa kinara wa asisti akiwa nazo 17 na akiifungia timu yake mabao 7.
Akizungumza na Championi Ijumaa, mzee Akilimali alisema kuwa Ajibu alianza kucheza Simba, hivyo si ajabu kumuona akirudi katika timu yake hiyo lakini anafurahi kwa kuondoka kwake kwani alikuwa hana mapenzi na Yanga.
“Ajibu alianzia Simba, mimi sioni ajabu kwa yeye kurudi huko, kwanza nimefurahi kwa kuondoka kwake kwani sasa hivi Yanga tunachofanya ni kukata mti na kupanda mti, Ajibu alikuwa kama kirusi kwa Yanga kwani alikuwa anacheza lakini siyo kwa mapenzi.
“Mapenzi yake yote yalikuwa Simba, hivyo alikuwa kama kirusi kwetu, niwashauri tu Wanayanga kuwa wasisikitike kwa kuondoka kwake.
“Kitamba cha unahodha kinafaa kurejeshwa kwa Kelvin Yondani kwani ni mchezaji mzuri, mimi nilishangaa kocha (Mwinyi Zahera) alipomvua unahodha na kumpa Ajibu lakini hatukutaka kuingilia kwani tulijua mwalimu atakuwa ameona kitu,” alisema Mzee Akilimali.