Akamatwa Kwa Kumhonga Rushwa Mkuu Wa Wilaya


TAKUKURU Mkoa wa Dodoma leo inatarajia kuwafikisha mahakamani watu saba (7) ambao tunawashikilia kwa kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)a na kuahidi na kutoa rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)b vyote vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Kwanza tunawashikilia wanaume wawili ambao ni Bw. Bahadur Abdalah Hirji (68), Mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Tembo Kata ya Madukani Jijini Dodoma na mwanaye Bw. Nahid Bahadur Hirji (33) ambaye ni Mhasibu wa kampuni ya Victory Bookshop Ltd ya Jijini Dodoma kwa kosa la kuahidi na kutoa hongo ya shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000/=) kwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Petrobas Paschal Katambi ili asifuatilie mapungufu katika utekelezaji wa amri ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Dodoma ya kukazia hukumu lililowasilishwa kwake na dada wa Bahadur Hirji.

Baada ya kupata taarifa ya watuhumiwa kuahidi kutoa fedha hiyo kama kishawishi kwa Mkuu wa Wilaya, tulianza kuwafuatilia na kufanikiwa kuwakamata tarehe 27 Julai, 2019 majira ya saa kumi na moja jioni katika Hoteli ya Royal Village, Area D Jijini Dodoma mara baada ya mtuhumiwa Nahid kumkabidhi Mkuu wa Wilaya rushwa hiyo.

Pia tunamshikilia Bw. Omary Said Mtauka ambaye ni Msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora iliyopo Jijini Dodoma ambaye aliomba na kupokea hongo ya Shilingi laki moja na elfu kumi (110,000/=) kutoka kwa Mzee mwenye umri wa miaka sabini na nane (78) aitwaye Paulo Mawope, mkazi wa Chilungule Kata ya Makutupora ili amalize tuhuma dhidi yake za kugombana na jirani zilizowasilishwa kwa Mtendaji wa Mtaa na baadaye ofisi ya Kata.

Awali, tulipokea taarifa kutoka kwa Mjukuu wa Mzee huyo kwamba alipigiwa simu na ‘Mtendaji wa Kata ya Makutupora’ akitakiwa kutoa fedha hizo ili babu yake aliyekuwa ameshtakiwa katika ofisi ya Kata aachiwe.

Uchunguzi wetu uliweza kuthibitisha uwepo wa suala la Mzee huyo kushtakiwa na jirani yake, kushikiliwa na kutakiwa kutoa fedha ili suala hilo limalizwe na tulifanikiwa kumnasa mtuhumiwa baada ya kupokea hongo hiyo majira ya saa mbili usiku wa tarehe 25 Julai, 2019 katika Bar ya Mama Lili iliyopo Makutupora Jijini Dodoma.

Baada ya kumkamata tulibaini Mtuhumiwa ni Msaidizi wa Mtendaji wa Kata ya Makutupora na alikamilisha uhalifu wake kwa kujifanya ni Mtendaji wa Kata.

Aidha, tunamshikilia Bw. Stanley John Motambi (34) ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Matumbulu kilichopo Kata ya Matumbulu Jijini Dodoma kwa kosa la kuomba na kupokea hongo ya shilingi elfu sitini na tano (65,000/=), kinyume na taratibu za utendaji, kutoka kwa ndugu za Bw. Wilfred Mnyambwa Mtundu ambaye alikuwa na shauri la mgogoro wa ardhi mbele ya Mtendaji wa Kijiji, kama kishawishi ili asikilize shauri hilo baada ya kutembelea eneo lenye mgogoro.

Baada ya kupata taarifa tulifanya uchunguzi na kuthibitisha kwamba Mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 3 Juni, 2019.

Watuhumiwa wengine ni Bw. Venance Msafiri Mayo (34) na Bw. Sulaith Abdul Rusheke (33) ambao ni walimu wa Shule ya Sekondari Viwandani iliyopo Kata ya Viwandani Jijini Dodoma ambao waliomba na kupokea hongo ya shilingi elfu ishirini (20,000/=) ili wampatie cheti cha utambulisho wa kusoma shule (leaving certificate) mtoa taarifa aliyekuwa mwanafunzi wa shule hiyo.

Awali, wakati mwanafunzi huyo alipotaka kuomba nafasi ya kozi fupi katika Taasisi fulani alitakiwa awasilishe cheti hicho hivyo akaenda shuleni hapo na ndipo watuhumiwa wakamtaka, kinyume na utaratibu, atoe rushwa ili wampatie cheti hicho na ndipo akatoa taarifa kwetu.

TAKUKURU ilifuatilia taarifa hiyo na majira ya saa nne na nusu asubuhi tarehe 26 Julai, 2019 kufanikiwa kumkamata Mtuhumiwa Mayo akiwa kwenye Bajaj yenye namba ya usajili MC686BHK iliyoegeshwa nje ya uzio wa shule baada ya kupokea hongo hiyo na kumkabidhi mhusika cheti.

Mtuhumiwa alienda katika eneo hilo akiwa na mhuri wa Mkuu wa Shule na cheti husika na alikigonga mhuri na kumpatia mtoa taarifa wetu baada ya kupokea fedha hiyo. Baada ya hapo tulimkamata pia Mtuhumiwa Rusheke kwani alishiriki katika kushawishi hongo hiyo.  Kiutaratibu vyeti hivyo vinatolewa bila gharama yoyote.

Mwingine ni Bw. Abdulhakim Abbas Kabunga (26) ambaye ni mtumishi wa muda wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dodoma ambaye tulimkamata mchana wa tarehe 27 Julai, 2019 baada ya kupata taarifa kwamba amepokea hongo ya shilingi elfu thelathini (30,000/=) kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa na uhitaji wa Kitambulisho cha Taifa ili amsaidie kukipata haraka.

Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa amekiri kuhusika na kitendo hicho na atafikishwa mahakamani leo.

Nawakumbusha wote wanaofuatilia vitambulisho vyao NIDA kwamba huduma hiyo ni bure na iwapo watatakiwa kutoa rushwa ili wahudumiwe mapema basi watupe taarifa mara moja.

Pia tunaendelea kuwakumbusha watumishi wote wa umma na wakazi wa Dodoma kwa ujumla kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa kwani sio tu kwamba vinaminya haki za wananchi bali pia havina nafasi kwenye mkoa wetu.

Aidha, tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kutupa taarifa na kuwasihi waendelee kuwa washiriki wa dhati katika vita dhidi ya rushwa ikiwa ni pamoja na kushiriki kutoa ushahidi mahakamani.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad