Mwanza. Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema kutenguliwa kwa uteuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) ni pigo kwa wananchi anaowaongoza katika jimbo lake.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Julai 21, 2019 Heche amesema Makamba ambaye ni mbunge wa Bumbuli (CCM) anapaswa kupewa zawadi kutokana na utendaji wake mzuri uliojaa ufanisi, akitolea mfano jinsi alivyosimamia katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki.
“Makamba alionyesha weledi wa hali ya juu katika kushughulikia suala la katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki. Mimi nilitarajia kupongezwa na kupewa zawadi,” amesema Heche.
Amesema wizara aliyokuwa akiisimamia Makamba ilifunga mgodi wa Nyamongo kutokana na kutiririsha maji yenye sumu yaliyokuwa yakielekea katika makazi ya watu na kusababisha athari kwa mifugo na uharibifu wa mazao.
“Mtu kama huyo anayejali maisha ya watu na kutoa suluhu ili kunusuru uhai wa binadamu usingetegemea kuona anatenguliwa,” amesema Heche.
Leo, Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa mawaziri wapya wawili, akimteua Hussein Bashe kuwa naibu Waziri wa Kilimo kuchukua nafasi ya Innocent Bashungwa ambaye hivi karibuni ameteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.
By Jonathan Musa, Mwananchi jmusa@mwananchi.co.tz