Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, imempatia msaada wa mashine ya kusaidia kupumua (Oxygen Concentrator) Bw. Hamad Awadhi kutokana na matatizo yake ya afya ambayo yanamlazimu kutumia mashine ya oxygen muda wote ili aweze kupumua.
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-MNH-Prof. Charles Majinge amesema hospitali imempatia msaada Bw. Awadhi kwa lengo la kuokoa maisha yake sanjari na kuimarisha afya yake lakini pia kumuwezesha kuendelea na shughuli zake za kawaida ili kutokua tegemezi kutokana na hali yake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru ameeleza kwamba mashine hiyo inathamani ya shilingi milioni tatu na nusu imenunuliwa na Hospitali ya Mloganzila ambapo wataalam wamempatia mafunzo Bw. Awadhi namna ya kuitumia na kuitunza ipasavyo.
Prof. Museru amemtaka Bw. Awadhi kuitunza na kuitumia vema mashine hiyo kama ambavyo ameelekezwa na wataalam ili afya yake itakapoimarika iweze kusaidia watanzania wengine.
“Hospitali imekupatia msaada wa mashine hii ya kukusaidia kupumua kwa lengo la kuhakikisha afya yako inaimarika zaidi hivyo tunaomba uitunze na utakapopona kabisa utairejesha hospitali ilituwasaidie wengine,” amesema Prof. Museru.
Naye Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani MNH- Mloganzila, Dkt. Patricia Munseri amesema, Bw. Awadhi kwa muda wote aliokuwepo hospitalini ameishi kwa kutegemea mashine ya oxygen ambayo inamsaidia kupumua ambapo kwa siku alikua akitumia gesi wastani wa lita 5,760.
Bw. Hamad Awadhi alifikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila Julai 9 mwaka 2018 na kuruhusiwa Julai 9 mwaka 2019 baada ya afya yake kuimarika.
Apatiwa Mashine ya kupumua baada ya kulazwa mwaka mmoja
0
July 10, 2019
Tags