Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mkazi wa Tabata Segerea, Daudi Iddy (23) kwa kujifanya ofisa wa polisi mwenye cheo cha mkaguzi msaidizi wa polisi.
Akizungumza leo Jumanne Julai 30,2019, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema Julai 19, 2019 jeshi hilo lilipata taarifa toka kwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Makao Makuu, Mlalakuwa jijini Dar es Salaam kuwa kuna kijana aliyevaa sare za jeshi la polisi wanamtilia shaka.
“Makachero wa jeshi la polisi walifika Makao Makuu ya JKT kumkamata na kufanya naye mahojiano, mtuhumiwa alikiri kujifanya yeye ni ofisa wa polisi na kufanya utapeli” amesema Kamanda Mambosasa
Amesema askari huyo feki pia alikiri kupata mafunzo JKT huko Mafinga mwaka 2006 na kujitolea kwa mujibu wa sheria katika kambi hiyo.
“Baada ya kufanyiwa upekuzi alipatikana na vifaa mbalimbali ikiwemo sare moja ya polisi, vyeo vya kapteni sajenti na cheo cha mkaguzi msaidizi, pingu, buti na viatu pamoja na redio ya upepo” ameongezaRead More: Nafasi za Ajira Serikalini Zilizotangazwa Leo
Kamanda Mambosasa amesema upelelezi wa kina unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.