Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki amesema alipomsikia Rais John Magufuli kuwaita wateule wake wapumbavu alishtuka na kwa sasa amegundua alikuwa sahihi.
Balozi Kagasheki aliandika ujumbe huo leo kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa awali alishtuka na kauli hiyo lakini alipoona mijadala ya hivi karibuni iliyoanzia BBC ameamini Rais Magufuli alikuwa sahihi.
Kagasheki ambaye aliwashawahi kuwa Mbunge wa Bukoba Mjini (CCM) aliandika ujumbe unaoseme hivi:
”Nilimuona Mhe Rais Kwenye runinga akiwataja baadhi ya wateule wake na kusema wakati mwingine hulazimika kuwapigia simu usiku na hata kuwaita wapumbavu nilishtuka lakini baada ya kuona maijadala hivi karibuni iliyoanzia BBC nimeamini Rais Magufuli alikuwa sahihi,”.
Nilimuona Mhe Rais kwenye runinga akiwataja baadhi ya wateule wake na kusema wakati mwingine hulazimika kuwapigia simu usiku na hata kuwaita wapumbavu. Nilistuka.Lakini baada ya kuona mijadala hivi karibuni iliyoanzia BBC, nimeamini Rais @MagufuliJP alikuwa sahihi. #KSK_Balozi— Khamis Kagasheki (@KKagasheki) July 12, 2019
Licha ya kwamba Balozi Kagasheki hakuweka wazi mijadala hiyo ni kwamba hivi Karibuni kulikuwa na mjadala mzito baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Palamagamba Kabudi kudai kuwa Mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda, alitoweka na kufariki.
Kauli hiyo ilizua utata katika mitandao ya kijamii huku wengine wakihoji waziri huyo amejuaje kama mwandishi huyo amefariki.
Waziri Kabudi aliyasema hayo wakati wa mahojiano na BBC katika kipindi cha FOCUS ON AFRICA mjini London waziri Kabudi alinukuliwa akisema kwamba visa vya watu kutoweka vimesababisha uchungu mwingi nchini humo.
“Wacha nikwambie unapozungumzia kuhusu kisa hicho, ni mojawapo ya visa ambavyo vimesababisha uchungu mwingi nchini Tanzania”.
Aliongezea kuwa :”Katika eneo la Rufiji sio tu Azory Gwanda aliyetoweka na kufariki, nataka kukuhakikishia kwamba tunachukua kila hatua sio tu katika eneo la Rufiji bali pia maeneo mengine ya Tanzania ili kuhakikisha kuwa watu wetu wako salama sio tu waandishi , bali pia Polisi na raia wa kawaida.
Kauli hiyo ilizua mjadala katika mitandao huku wakimtaka aonyeshe maiti hiyo ilipo kwani haijawahi kutolewa hiyo taarifa na familia yake haijui kama alishakufa.
Baada ya mjadala huo kupamba moto Waziri Kabudi alikanusha alikanusha taarifa hizo huku akidai vyombo vya habari vimemnukuu vibaya.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa potofu zinazoendelea kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii ikinukuliwa kimakosa mahojiano yangu kwenye Kipindi cha BBC FOCAS ON AFRICA zikidai kuwa nimethibitisha kwamba Azory Gwanda amefariki dunia,”
Naye Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abbas amesema mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda amekufa ama yupo hai na kwamba vyombo vya usalama vinaendelea na uchunguzi.
Licha ya serikali kukanusha taarifa hizo baadhi walisema ni vyema Waziri Kabudi akaomba radhi yakaisha kuliko kukataa maneno aliyoyatamka huku wakiendelea kusambaza video inayoonyesha alitamka maneno ya kwamba Azory alitoweka na kufariki.