Bashe ametoa kauli hapo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo alisema tamko la makatibu wakuu hao wastaafu walilomuandikia katibu wa baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu, Pius Msekwa, limekwenda kinyume cha Katiba ya CCM.
Pia, ameeleza kuwa "Wao wenyewe wamesema kuwa hawamtafuti Musiba bali anayetoa kinga, sasa mimi sipendi kumumunya wala kuzunguka mambo hapa wanamlenga Rais Magufuli"
“Hatuwezi kuruhusu Magufuli ni mwenyekiti wetu, ni mgombea wetu wa urais 2020, come sun come rain (lije jua ije mvua), hatuwezi kuruhusu hatua ambayo inadhoofisha uhai wa chama,” amesema Bashe.
Ametaja kifungu 122 (1) cha Katiba ya CCM akisema kimekiukwa na tamko hilo kwa kuwa baraza hilo halina mamlaka ya kusikiliza malalamiko hayo.
“Ukiwa na malalamiko lazima ujue wa kumwandikia. Mimi nikilalamikia gazeti namwandikia editor (mhariri) ndio ana mamlaka ya kisheria, siwezi kumwambia circulation manager (meneja usambazaji),” amesema Bashe.
Amebainisha kuwa kosa jingine lililofanywa na makatibu hao kwenye waraka wao ni kuuweka hadharani.
Amesema "Wanajua vizuri Katiba, miiko na tamaduni za Chama chetu, na kwamba unapeleka malalamiko ya mwanachama kwenye chama, Musiba si mwanachama wa CCM"
Amebainisha kuwa njia nzuri ambayo akina Kinana wangetumia ni kutumia bazara lao la Wastaafu na kuongea kule kwani pia wana uwezo wa kumuita Rais au kumfuata Ikulu kuongea naye
Hata hivyo amesema kuwa linapokuja suala la CCM ni lazima waungane na kusema kuwa Mzee Msekwa anaelewa kilichofanywa na akina Kinana ni kinyume na Katiba na ndio maana amesema suala hilo amepeleka kwenye chama