Bashe "Hatua ya Kinana ni ya ovyo ni Mkakati Unaolenga Kumkosesha Uhalali Rais 2020"


Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini (ccm), Hussein Bashe amesema walichokifanya makatibu wastafu wa CCM, Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana ni hatua za kutaka kumkosesha Rais John Magufuli asigombee urais mwaka 2020.

Bashe aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa malalamiko yao waliyoyawasilisha katika Baraza la Ushauri la Viongozi wakuu wastaafu wa chama hicho ni maamuzi ya ovyo kuliko mambo anayofanya Cyprian Musiba.

Bashe alisema nia yao ni kutaka kukigawa chama chao na jambo la pili ni kumgawa Rais John Magufuli na jambo la tatu kukigawa chama hicho katika uchaguzi, hivyo hawawezi kuruhusu hicho kinachoendelea.

Magufuli ni mgombea wao wa Urais mwaka 2020 hawawezi kuruhusu hatua yoyote ambayo inadhoofesha umoja na mshikamano wa chama chao.

Makamba na Kinana waliwasilisha malalamiko yao dhidi ya Cyprian Musiba na kuliomba baraza hilo kumshughulikia kwani amekuwa akiwatuhumu kukwamisha jitihada za Rais John Magufuli.

Viongozi hao wastaafu katika waraka wao walioutoa walisema wanashangazwa kwanini Musiba achukuliwe hatua licha ya kwamba anatumia lugha za vitisho na kuhatarisha usalama wa raia hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake.

Walisema kwa muda mrefu amejitokeza mtu anayejitambulisha kama ni mwanaharakati na mtetezi wa Rais John Magufuli na kuwatuhumu kwa mambo ya uzushi na uongo.

“Tumetafakari kwa kina na kuamua kutoa taarifa hii kwa umma kuhusiana na Musiba dhidi yetu. Watanzania wanajua haya anayoyasema mtu huyu kuhusu watu mbalimbali sio ya kwake anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu. Huyu ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi yetu katika mazingira haya hatuwezi kukaa kimya,”

Viongozi hao wamesema wameandika barua kwa katibu wa Baraza la ushauri la viongozi wakuu wastaafu CCM, Mzee Pius Msekwa, Baraza ambalo mwenyekiti wake ni Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi, Rais na Mwenyekiti mstaafu wa CCM.

Wamesema wanafanya hivyo kwa kufuata katiba ya CCM toleo la 2017 ibara ya 122 wamewasilisha na maombi yao kwa wazee hao kutumia busara zao katika kulishughulikia jambo hilo ambalo linaelekea kuhatarisha umoja, ushikamano na utulivu ndani ya chama na nchi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad