Bilionea Amwaga Bilioni 1.3 Yanga

KAMPUNI ya GSM Group Limited inayomilikiwa na bilionea Ghalib Mohammed imefanya kufuru nyingine Yanga, ni baada ya kushinda tenda ya utengenezaji jezi kwa kitita cha shilingi bilioni 1.3 watakazozitumia kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Hiyo, ni mara ya tatu kwa kampuni hiyo kuimwagia Yanga fedha ambayo walianzia kwenye sherehe za ‘Kubwa Kuliko’ ambapo walichangia shilingi milioni 300, pia walilipia shilingi milioni 15 kwa ajili ya ukumbi wa Diamond Jubilee, Upanga ilipofanyikia shughuli hiyo.

GSM wiki mbili zilizopita ndiyo ilitangazwa kushinda tenda ya utengenezaji wa jezi hizo za msimu ujao baada ya kuzishinda kampuni mbili ikiwemo Vunja Bei.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, GSM chini ya mwenyekiti wake, Ghalib Mohammed, imeshinda tenda hiyo baada ya kuzishinda kampuni hizo ambazo zote ziliweka mezani dau dogo la shilingi milioni 200 kila moja.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, GSM tayari wamekabidhiwa tenda hiyo ya utengenezaji wa jezi zitakazotumika kuvalisha wachezaji za mechi ya nyumbani na ugenini ambazo zitatambulishwa Agosti 4, mwaka huu kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.

“Maneno mengi yamejitokeza baada ya GSM kutangazwa kuwa wameshinda tenda ya utengenezaji wa jezi za msimu ujao wa ligi kwa wachezaji wetu. “Jezi hizo zitatumika kuvaliwa na wachezaji wetu ambazo zitakuwa za nyumbani, ugenini na zile za mazoezi, pia zitakuwepo jezi za mashabiki ambazo zitatambulishwa kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi.

“GSM wameshinda tenda hiyo ya jezi baada ya kutoa kitita cha shilingi bilioni 1.3 ambazo ziliwashinda washindani wenzake waliokuwa wanashindanishwa katika tenda hiyo ambao wote walikuwa na shilingi milioni 200,” alisema mtoa taarifa huyo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad