Kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya huduma za Usafirishaji wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (UDART), Robert Kisena na Wenzake wanne, imepigwa tena kalenda katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu, hadi itakaposikilizwa tena Julai 15, 2019 baada ya upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 38 ya mwaka 2019, leo Julai 5 ilifikishwa Mahakamani hapo, kwa lengo la kusikiliza shauri la upepelezi kutoka upande wa mashtaka, ambapo upelelezi haujakamilika na watuhumiwa wote wamerudishwa rumande.
Kisena na wenzake wanakabiliwa na mashtaka 19, yakiwemo ya utakatishaji fedha na kuisababishia UDART hasara ya shilingi bilioni 2.
Wakili wa Serikali Elizabeth Mkunde, ameieleza tena Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile kuwa upelelezi haujakamilika. Baada ya maelezo hayo, Hakimu Rwezile ameiahirisha kesi hiyo hadi Julai 15 itakapotajwa tena.
Mbali na Kisena, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mke wa Kisena, Florence Mashauri, Kulwa Kisena, raia wa China Chen Shi na Mhasibu wa Kampuni hiyo Charles Selemani Newe. Katika kesi ya msingi, washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2011 na Mei31, 2018, ndani yajiji la Dar Es Salaam waliongoza genge la uhalifu.
Mashtaka mengine ni kufanya biashara katika eneo ambalo halijaruhusiwa, kuiba shilingi bilioni 1.2 mali ya UDART huku mashtaka manne yakiwa ni ya utakatishaji wa fedha.