Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenarali Marco Gaguti, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani humo, kuhakikisha inawachukulia hatua watumishi wote waliohusika na ubadhilifu wa fedha za umma katika Halmashauri, ikiwemo kuwakata mishahara yao.
Gaguti ametoa maagizo hayo katika hotuba yake iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, kwenye kikao maalumu cha kujibu hoja za CAG, kilichofanyika wilayani hapo ambapo Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Sada Malunde ndiye aliyewasilisha hoja hiyo kwa Mkuu wa Mkoa Gaguti.
Kwa mujibu wa Gaguti jumla ya hoja 81 ziliibuliwa katika ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, (CAG) Prof. Mussa Assad, ikiwemo malalamiko ya matumizi mabaya ya fedha za umma pamoja na kukua kwa deni la Halmashauri hiyo.
RC Gaguti ametoa siku mbili kurejeshwa kwa fedha ambazo zimetumika kinyume na malengo na kueleza endapo fedha hizo hazitarejeshwa, Halmashauri hiyo haitasita kuwakata mishahara yao.