Profesa Assad aliyasema hayo jana katika kongamano la maadhimisho ya siku maalumu ya kutafakari mapambano dhidi ya rushwa iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) ikishirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Kongamano hilo lilifanyika katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu sabasaba, viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Profesa Assad alisema endapo kutakuwa na uwazi katika kila jambo, ikiwemo tenda mbalimbali na masuala ya ajira nchini, rushwa itakwisha.
“Hakuna asiyefahamu kuwa mwarobaini wa rushwa ni uwazi, hasa katika tenda mbalimbali kwenye sekta za umma na hata ajira, kukiwa na uwazi tatizo la rushwa litakwisha,” alisema Profesa Assad.
Katika kongamano hilo kulijadiliwa mada tatu ambazo ni mwelekeo wa Serikali katika mapambano dhidi ya rushwa, wajibu wa sekta binafsi katika mapambano hayo na athari za rushwa katika uchumi.