Daktari Atoa Ushahidi Kesi Ya Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA

Shahidi wa tano, Inspekta Msaidizi Dk. Juma Alfani (54) katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake, amedai mahakamani kwamba aliwapokea Koplo Rahim na Konstebo Fikiri wakiwa wanapiga kelele za kulalamika maumivu ya majeraha waliyopata kwenye maandamano.

Kadhalika, amedai kuwa Koplo Rahim alikuwa anaweweseka huku akilalamika maumivu shingoni kwa sababu alikuwa hajitambui na Konstebo Fikiri alikuwa anavuja damu nyingi kichwani.

Madai hayo aliyatoa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba, wakati akisikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya vigogo tisa wa Chadema.

Jopo la Jamhuri liliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Dk. Zainabu Mango, Mawakili wa Serikali Jacqueline Nyantori, Wankyo Simon na Salimu Msemo.

Akiongozwa na Wakili Msemo, shahidi alidai kuwa Februari 16, mwaka jana, alikuwa kazini zamu ya usiku.

"Saa 5:40 usiku nikiwa wodi ya wazazi alikuja muuguzi wa zamu akaniarifu nahitajika kitengo cha dharura. Nilipokwenda niliwakuta wagonjwa wawili mmoja akivuja damu, huku akipiga kelele za maumivu na mwingine akiwa anaweweseka hana fahamu," alidai.

Aliongeza katika ushahidi wake kuwa: "Niliwaagiza wauguzi wawachome sindano za maumivu, nikamhoji aliyekuwa anatokwa damu kichwani, Fikiri kimetokea nini, akanieleza walikuwa wanatuliza maandamano ndipo wakajeruhiwa.

“Nilipojaribu kumhoji Rahim alikuwa anaweweseka na kuonyesha maumivu kwenye shingo upande wa kulia," alidai Dk. Alfani ni daktari wa Hospitali ya Polisi Barabara ya Kilwa ambayo ni ya rufani kwa zahanati zote za polisi.

Alidai kuwa baada ya kuwakagua majeruhi na kujiridhisha aliagiza wapelekwe wodini na walilazwa mpaka Februari 18, mwaka jana waliporuhusiwa. Pia alidai kuwa baada ya Rahimu kuendelea kulalamika maumivu aliagiza akafanyiwe kipimo cha CT Scan. Kesi hiyo inaendelea leo kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri.

Jopo la utetezi liliongozwa na Wakili Profesa Abdallah Safari, Peter Kibatala, John Mallya na Hekima Mwasipu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Katibu Mkuu wa Chadema, Vicent Mashinji; Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu Mbowe na wenzake wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana, Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyoko Kinondoni, Dar es Salaam kwa kuwataka wakazi wa eneo hilo kufanya maandamano yenye vurugu.

Pia ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka jana katika barabara ya Kawawa eneo la Konondoni Mkwajuni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad