Arsenal imeipiku Tottenham katika kumsajili beki wa klabu ya Ufaransa ya Saint Etienne William Saliba kwa dau la £27m, siku ambayo kiungo wa kati wa Real Madrid Dani Ceballos pia alijiunga na klabu hiyo kwa mkopo.
Salliba mwenye umri wa miaka 18 ametia saini kandarasi ya miaka mitano lakini ataendelea kuichezea klabu hiyo ya daraja la kwanza msimu ujao kabla ya kujiunga na Arsenal 2020.
Mchezaji wa Uhispania Ceballos amejiunga kwa mkataba wa muda mrefu msimu huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ameichezea Real madrid mara 56 tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Uhispania kutoka Real Betis.
Kuhusu usajili huo wa mkopo, mkufunzi wa Arsenal Unai Emery alisema: Tunafurahia Kuona Dani amejiunga nasi. Ni mchezaji mwenye talanta akiwa na uwezo wa kiufundi , mbunifu na pasi sahihi.
Ceballos aliichezea nchi yake mara sita , atavaa jezi nambari nane msimu huu na huenda akaanzishwa mara ya kwanza katika kombe la Emirates dhidi ya Lyon siku ya Jumapili.
Usajili wa Salliba unatokana na hamu ya Arsenal tangu 2018 na unajiri licha ya ushindani mkali kutoka kwa Tottenham.
Kurudi Saint Etienne kwa kinda huyo wa timu ya Ufaransa yalikuwa makubaliano yasio na mbadala.
''Tunafurahia kwamba Williama atajiunga nasi'' ,alisema Emery. ''Klabu nyingi zilimtaka lakini akaamua kuja kwetu na kuwa katika timu yetru ya siku zijazo''.
''Atasalia Ufaransa msimu ujao ili kupata uzoefu zaidi na baadaye tutaangalia njia za yeye kujiunga na kikosi chetu''.