Dar es Salaam. Mwanamuziki Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ametajwa katika mkutano mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi.
Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia amelitaja jina la Diamond wakati akizungumzia jinsi mabadiliko ya teknolojia yanavyoweza kuwafanya watu kupata taarifa ndani ya muda mfupi, zikiwemo nyimbo za wanamuziki mbalimbali akiwemo Diamond.
Katika mkutano huo unaofanyika leo Jumamosi Julai 27, 2019 jijini Dar es Salaam, Mbatia amesema nyimbo za Diamond kwa sasa zimesambaa kwa kasi nchini, zikiteka kundi kubwa la vijana wanaoziimba kila mahali kutokana na kasi ya usambazaji wa taarifa.
Mbatia amesema kasi ya ukuaji wa mabadiliko ya teknolojia ya habari imechagiza kuongezeka kwa kiwango cha upatikanaji wa taarifa, kuzungumzia umuhimu wa Taifa kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia kwa wakati sahihi wananchi.
“Je ni taarifa sahihi wanapata na wanazichambua namna gani. Juzi Diamond ametoa wimbo wake ndani ya saa 48 yuko kule Tabora, kule vijijini watoto wa shule za msingi, sekondari wanaimba huwezi kuamini ni watu wa kijiji wanaimba wimbo za Diamond wa Dar es Salaam, ni taarifa zinavyoenda kwa kasi, “ amesema Mbatia.
Mbatia alianza kwa kugusia vipaumbele vilivyopo katika malengo endelevu matatu ya chama hicho ambayo ni kuondoa umaskini, njaa na afya pamoja na mahitaji ya taarifa kwa kundi kubwa la vijana.