Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, ametangaza kiama kwa wavuvi haramu waliohusika katika mauaji ya watu wanne, akiwemo ofisa mfawidhi wa rasilimali za uvuvi kanda ya Ukerewe yaliyotokea hivi karibuni.
Waziri Mpina amesema hayo, wakati akiongoza waombolezaji kuaga mwili wa Ofisa Mfawidhi aliyeuawa katika mapambano kati ya wananchi na maofisa wa kikosi cha kupambana na uvuvi haramu wa kanda hiyo.
''Natangaza vita haramu, vita mpya na tutawasaka kila mahali, tutaimarisha sekta zote kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa na hata mkiniua leo atateuliwa waziri mwingine, hamuwezi kupona kwa kutumia nguvu'' amesema Mpina.
Waliofariki katika mapambano hayo ni Ofisa Mfawidhi wa rasilimali za uvuvi kanda ya Ukerewe, Ibrahim Nyangali (38), na wakazi wa kisiwa hicho ambao ni, Damian Joseph (18), Malanja Malima (18) na Chrisant Christian (47).
Aidha Waziri amesema wavuvi haramu hawawezi kushindana na Serikali na alitangaza kuanza oparesheni ya kuwasaka wavuvi haramu iliyoanza jana Julai 24.