ICC Yamtia Hatiani Kiongozi wa zamani wa waasi kwa Makosa ya Uhalifu wa Kivita


Kiongozi wa zamani wa waasi amekutwa na hatia kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hukumu iliyotolewa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC).

Bosco Ntaganda, aliyejulikana kwa jina ''Terminator'', alishtakiwa kwa makosa ya mauaji, ubakaji na kuwasajili watoto kwenye jeshi.

Mawakili wake wamesema kuwa Ntaganda mwenyewe ni muathirika kwa kuwa alisajiliwa kwenye jeshi akiwa mtoto.

Ntaganda amekuwa mtu wa nne kuhukumiwa na ICC tangu kuundwa kwake mwaka 2002.

Wachambuzi wamesema ni kitendo cha kujilinda, kutokana na hatari iliyokuwa ikimkabili hasa baada ya kushindwa mzozo wa kugombea uongozi ndani ya kundi la waasi wa M23.

'Terminator' ni nani

Alizaliwa mwaka 1973, na kukulia nchini Rwanda
Alitorokea DRC akiwa kijana baada ya mashambulizi dhidi ya watu wa kabila ya Tutsi
Akiwa na umri wa miaka 17 alianza kupigana akiwa muasi na mwanajeshi , nchini Rwanda na DRC
2009: Aliingia jeshi la taifa la DRC na kuwa Jenerali
2012: Aliasi jeshi, hali iliyozusha uasi mpya ambapo watu 800,000 walikimbia makazi yao
2013: Alijisalimisha kwenye ubalozi wa Marekani mjini Kigali, baada ya kugawanyika kwa kundi lake la uasi
Majaji walimkuta na hatia Ntaganda kwa makosa 18 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu uliotokea katika mji wa mashariki wa Ituri mwaka 2002 na 2003.

Ntaganda, 45, ''kiongozi mkuu'' alikuwa akitoa amri ''kuwalenga na kuwaua raia'' Jaji Roberrt Fremr amesema kwenye hukumu .

Waendesha mashtaka wamesema Ntaganda alipanga na kuongoza operesheni ya waasi wa Union of Congolese Patriots (UCP) na tawi lake la kijeshi, la Patriotic Forces for the Liberation of Congo (FPLC).

Amekutwa na hatia kuhusika na vitendo vya ubakaji na utumwa wa kingono. Majaji pia wamesema Ntaganda mwenyewe alimuua kasisi wa kikatoliki.

Uhalifu huu ulifanyika wakati Ntaganda alipokuwa kiongozi wa kundi la waasi lililokuwa chini ya Thomas Lubanga, kiongozi wa waasi wa UPC. Alihukumiwa na ICC mwaka 2012.

Majaji wamemkuta na hatia Ntaganda kwa uhalifu wa kuwasajili watoto kwenye jeshi, wakiwemo wasichana.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad