Mtandao wa Instagram unaamini kuwa kuwepo kwa ujumbe wa kuwafanya watumiaji wa mtandao kufikiri kuhusu wanachokisema, utasaidia kuondokana na vitendo vya udhalilishaji mtandaoni.
Hivi karibuni itawapatia watu wanaodhalilishwa mitandaoni uwezo wa kuzuia majibizano na watumiaji wanaowadhalilisha.
Instagram imekuwa kwenye changamoto ya kupambana na tatizo la udhalilishaji baada ya madhara makubwa kutokea kama tukio la kujiua kwa binti mmoja wa nchini Uingereza.
''Tunaweza kufanya zaidi kuepuka vitendo hivi kufanyika kwenye instagram, na tunaweza kuchukua hatua zaidi za kuwawezesha walengwa wa vitendo hivyo ili waweze kujitetea wenyewe''.ameeleza mtendaji mkuu Adam Mosseri.
Instagram imesema imekuwa ikitumia teknolojia ya kubaini kama ujumbe unafanana na aina ya ujumbe unaowekwa ambao umekuwa ukiripotiwa kuwa usiofaa kwa watumiaji.
Katika mfano mmoja, mtu ataandika ''wewe ni mbaya na mpumbavu.'' kisha ujumbe utamfikia kutoka instagram ukimuuliza: ''Una uhakika unataka kuweka ujumbe huu? fikiri zaidi''.
Ikiwa mtumiaji atabofya palipoandikwa ''fikiri zaidi'' ujumbe utatokea ukisema '' tunauliza watu kufikiri kuhusu kauli zinazoonyesha kufanana na zile zinazoripotiwa kuwa mbaya.''
Haki miliki ya pichaFAMILY HANDOUT/PA WIRE
Mtumiaji anaweza kupuuza ujumbe na kuweka ujumbe wake, lakini Instagram ilisema kwa majaribio ya awali yanaonyesha kuwa wataweza kuwafanya watu kufuta ujumbe mbaya na kuandika kitu kingine kisichomuudhi mtu ikiwa watakuwa na nafasi ya kutafakari.
Uwezo huo unaanzia kwa nchi za watu wanaozungumza kiingereza,kukiwa na mipango ya huduma hiyo kufika duniani kote, Instagram imeiambia BBC.
Mipaka
Kampuni imesema pia itakuja na kifaa kingine, kiitwacho Restrict (zuia),kilichoundwa kusaidia watoto kuchuja maneno bila kuwafungia wanaowadhalilisha hatua ambayo imeripotiwa kuleta matokeo chanya kwa dunia.
''Tumewasikia vijana kwenye jamii yetu kuwa wamekuwa wakishindwa kuwafungia, au kuwaondoa kwenye orodha ya marafiki au kuripoti vitendo vyao vya udhalilishaji wakihofu kuendelea kwa vitendo hivyo, alisema Mosseri.