WALLACE Karia, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania amesema kuwa kwa sasa bado wanaendelea kuzungumza na mdhamini mkuu ili kukamilisha utaratibu wa kufanya naye kazi.
Msimu uliopita Ligi Kuu iliendeshwa bila kuwa na mdhamini mkuu, TFF waliahidi kuwa msimu huu watakamilisha suala la mdhamini mkuu.
Karia amesema kuwa TFF inatambua thamani ya kuwa na mdhamini na wanazingatia vigezo kutokana na thamani ya ligi.
"Thamani ya ligi yetu ni kubwa hivyo hata mdhamini mkuu naye anapaswa awe mkubwa, hivyo bado tunapambana kumpata mdhamini mkuu kwa ajili ya msimu mpya.
"Pia napenda kuziomba timu ziweze kujiboresha ili kuvutia wadhamini ambao wataweka nembo yao mbele ya jezi kwani tuliboresha kwa upande wa mdhamini mkuu yeye anaweka upande wa mikono na mbele panabaki tupu kwa ajili ya mdhamini wa klabu," amesema.