Hatimaye viongozi wa jeshi la Sudan leo wamekubaliana na viongozi wa umoja wa vyama vya upinzani kuchangia madaraka hadi uchaguzi mwingine wa kidemokrasia utakapofanyika.
Pande hizo mbili zimekubaliana kuwa na wawakilishi katika ngazi zote za juu za Serikali kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Pia, wamekubaliana kuunda Serikali inayowahusisha wataalam na wanazuoni ambayo itaanza kwa kufanya uchunguzi wa vurugu zilizokuwa zimejitokeza katika kipindi cha wiki za hivi karibuni.
Taarifa za makubaliano hayo zimeamsha shamrashamra kwa wananchi katika mitaa ya majiji na miji ya nchi hiyo, kwa mujibu wa Aljazeera.
“Tunatumaini kuwa huu utakuwa mwanzo mzuri kwa ajili ya faida ya Wasudan wote,” alisema Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forces for Freedom and Change (FFC), Omar al-Degair.
Naye kiongozi wa Baraza la Mpito la Jeshi, Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo alisema, “makubaliano haya yatawahusisha watu wote, hakuna hata mmoja ambaye atatengwa. Tunawashukuru viongozi mbalimbali wa Afrika hususan Ethiopia kwa juhudi zao pamoja na uvumilivu wao katika kuhakikisha tunafika hapa.”
Awali, Jeshi la nchi hiyo lilikuwa na kigugumizi kuhusu kuruhusu viongozi wa umoja wa vyama vya upinzani kuunda Serikali ya kiraia. Walisema nchi hiyo itaongozwa na viongozi wa kijeshi kwa kipindi cha miaka mitatu wakati wanafanya maandalizi ya uchaguzi mkuu.
Sudan imekuwa katika vurugu tangu Jeshi la nchi hiyo lilipomuondoa madarakani aliyekuwa rais, Omar al-Bashir.
Bashir aliiongoza Sudan tangu Juni, 1989 alipofanikiwa kuipindua Serikali iliyokuwa madarakani. Mwaka huu, wananchi walianzisha maandamano makubwa ya kupinga utawala wake na kusababisha jeshi kumuondoa madarakani.