Kibabage: Afichua Siri na Msuva Pale Morocco, Kapagawa Aisee


SOKO la wachezaji wa Bongo limezidi kupanua wigo kwenye nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Marekani kutokana na kufanya vizuri na kuboresha viwango uwanjani.
Hatua hiyo ni mwanga mpya wa matumaini ya soka la Tanzania pamoja na timu ya Taifa, Taifa Stars, ambayo imekuwa ikipigiwa chapuo kuwa na mastaa wengi wanaocheza soka nje ya nchi ili kupata ujuzi na uzoefu mpya.
Hivi karibuni beki Nickson Kibabage aliyekuwa anakipiga Mtibwa Sugar, ametua kwenye klabu ya Al Jadida inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco.
Kutua kwa Kibabage kwenye chama hilo kunaongeza idadi ya Watanzania kwani, Simon Msuva ndiye anaongoza safu ya ushambuliaji na tayari ametengeneza rekodi zake tamu na kuwa tegemeo klabuni hapo.
Mwanaspoti lilizungumza na Kibabage, ambaye tayari ameanza kujifua kwa ajili ya msimu mpya akiwa sambamba na Msuva.

MAPOKEZI KWAKE FRESH TU
Kwa kawaida mgeni anapofika sehemu tofauti hukutana na changamoto za hapa na pale huku wengine wakiwa wapweke kutokana na mazingira.
Kwa upande wa Kibabage, ambaye ameichezea timu ya vijana chini ya miaka 17 na 23, alisema mapokezi yake yamekuwa mazuri tofauti na alivyokuwa anategemea.
“Mazingira yapo vizuri na nimepokelewa kama mchezaji wa kulipwa, ni kitu kizuri na kimenipa nguvu ya kupambana,” alisema.

MSUVA MBONA SAFI TU
Unakumbuka vile ambavyo Thomas Ulimwengu alipokelewa na Mbwana Samatta pale TP Mazembe na kuanza kuishi wote kule DR Congo?.
Basi ndivyo ilivyo hivi sasa katika kikosi cha Al Jadida baada ya Msuva kumpokea Kibabage na kuamua kukaa naye kwenye mjengo wake pale Morocco.
Kibabage alisema hayupo katika hostel za timu kwani, baada ya kufika Morocco moja kwa moja alipokelewa na Msuva na kukaa naye.
“Msuva ananichukulia kama mdogo wake wa damu, yupo fresh kiukweli yaani kifupi naweza kusema ni mzungu wa kupitiliza,” alisema.
Aliongeza kuwa wanavyoishi ndani ya nyumba ni kama ndugu hakuna kukwaruzana kwa vitu vidogo vidogo.

APEWA SIRI ZA KUTAMBA MOROCCO
Hakuna ambaye hajui Msuva amejitengenezea umaarufu wake pale Al Jadida, lakini umaarufu huko kunatokana na kufanya vizuri ndani ya uwanja, jambo ambalo kila mmoja analiona.
Kibabage anafichua kuwa baada ya kukaa na Msuva amemtonya namna ambavyo anatakiwa kuishi na kufanya kazi ili kuwa staa mkubwa.

MOROCCO NJIA TU
Tunaona Samatta alivyojitengenezea njia ya kutoka Simba, Mazembe mpaka Genk lakini bado kuna safari nyingine inataka kuanza ya kuchomoka katika kikosi hiko.
Msuva tumeona namna ambavyo ametoka Yanga na kwenda Al Jadida, licha ya kuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja inatajwa kuna timu zimepeleka ofa ya kutaka kumchomoa.
Kwa Kibabage naye baada ya kutua Al Jadida, amepiga hesabu zake na kuona kabisa sehemu hiyo ni sahihi kwa yeye kwenda kukipiga Ulaya.
“Nina malengo ya kucheza Ulaya na hilo ndio jambo langu kubwa, hapa ni njia tu muda utafika wa kwenda ninapopataka, sitoangalia nchi lakini Ulaya ni Ulaya tu,” alisema.

   
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad