Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla, amemuomba msamaha Waziri wa Mazingira, Mhe. Januari Makamba baada ya mvutano waliokuwa nao katika mtandao wa kijamii wa Twitter.
Majibizano hayo yalianza baada ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kudai kuwa inatarajia kuanzisha usafiri mpya wa kutumia magari ya umeme yanayopita kwenye nyaya (Cable Cars), kwa ajili ya kupeleka watalii katika mlima Kilimanjaro.
Waziri Makamba aliamua kujibu kwa kuandika, ''inabidi watu wa Mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza kabla hawajaanza. Na tutafanya 'studies' ili kujua madhara kwa mazingira na uthabiti wa 'mitigation measures".
Baada ya hapo, Waziri Kigwangalla alikuja tena na kutoa maelezo ya pili kuhusu TANAPA, "hivi kuna nchi ngapi zimeweka Cable Cars kwenye milima yake?, hizi haziharibu mazingira?, Cable inapita juu inaharibu mazingira gani?. Zaidi ya hekari 350,000/- za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni risk kubwa? ‘Watu wa mazingira’ wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu?".
Na leo Julai 8, 2019, kupitia ukurasa wake, Waziri Kingwangalla ameamua kumaliza malumbano hayo akikiri kuwa hakukuwa na haja ya kupeleka Twitter mjadala huo.
''Ni Jumatatu njema. Tunaanza upya. Tufunge. Mtani wangu Mhe. January Makamba anajua wazi kuwa kila mradi tunaofanya unafanyiwa EIA, hakukuwa na haja ya kuleta twitani jambo lile, lakini yameisha. All good. Tusameheane kwa yote. Wakimbu wangu walikaa vibaya jana nili-overreact!''