Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla ameonesha kutoridhishwa na kauli ya Waziri wa Mazingira, January Makamba akiieleza TANAPA kuwa hawawezi kuanza utaratibu wa kutumia magari maalumu ya umeme (Cable Cars), kwa ajili ya watalii wanaotembelea mlima Kilimanjaro.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri Kigwangalla amehoji baadhi ya maswali kwenda kwenye mamlaka ya mazingira, akieleza kuwa watu hao wamekuwa wakishiriki zaidi kwenye makongamano na si uhalisia wa kulinda mazingira.
"Watu wa mazingira wanataka kuingilia kati mradi wa cable cars KILIMANJARO. Lengo letu ni kukuza utalii, kuongeza mapato na kuboresha experience ya watalii wetu nchini. Tusipokuwa wabunifu tunatukanwa kutokutumia vizuri vivutio vyetu, tukiamka wanakuja ‘speed governors’.
"Hivi kuna nchi ngapi zimeweka Cable Cars kwenye milima yake?, hizi haziharibu mazingira?, Cable inapita juu inaharibu mazingira gani?. Zaidi ya hekari 350,000 za misitu zinapotea kila mwaka nchini, ipi ni hatari kubwa?, watu wa mazingira wamechukua hatua gani zaidi ya makongamano tu?", amesema Kigwangalla.
Hivi karibuni wakati TANAPA ilieleza mpango wake wa kuja na namna mpya ya usafiri kwa watalii wanaotaka kwenda kutembelea mlima Kilimanjaro, Waziri wa Mazingira, January Makamba akasema suala hilo haliwezi kufanyika mpaka pale NEMC watakapo thibitisha.
"Inabidi watu wa Mazingira tupitishe na kutoa cheti kwanza kabla hawajaanza. Na tutafanya 'studies' ili kujua madhara kwa mazingira na uthabiti wa 'mitigation measures", alisema Makamba