Klabu ya Liverpool ipo mbioni kuzipiku Real Madrid na Paris St-Germain kumsajili Harvey Elliott

Klabu ya Liverpool ipo mbioni kuzipiku Real Madrid na Paris St-Germain kumsajili kinda machachari kutoka klabu ya Fulham Harvey Elliott.

Elliott aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kukipiga kwenye Ligi ya Primia alipoingia kama mchezaji wa ziada kwenye mchezo wa Fulham dhidi ya Wolverhampton Wanderers mwezi Mei akiwa na umri wa miaka 16 na siku 30.

Hawezi kuwa mchezaji wa kulipwa mpaka atakapotimu umri wa miaka 17, ambayo itakuwa ni Aprili mwakani.


Inatarajiwa kuwa nyota huyo atakataa ofa ya masomo ya kuendelea kusalia katika klabu ya Fulham yenye maskani yake kwenye uwanja wa Craven Cottage ili aungane na mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya, klabu ya Liverpool.

Ikiwa, kama inavyotarajiwa, Liverpool wakamsaini Elliot, basi itawabidi wailipe Fulham fidia nono kwakuwa mchezaji huyo anayechezea pia timu ya taifa ya chini ya miaka 17 ya England anaonekana kuwa lulu ya baadae.

Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Elliott, ambaye pia amekuwa akiwindwa na Arsenal na Manchester City atakuwa ni nyota wa pili chipukizi kujiunga na Liverpool katika dirisha hili la usajili.

Tayari Majogoo hao wa jiji wameshamsajili beki kinda raia wa Uholanzi Sepp van den Berg aliyehamia kutoka klabu ya PEC Zwolle.

Liverpool imekwishalipa kitita cha awali cha pauni milioni 1.3 kumsajili Van den Berg, na yawezekana kitita hicho kikaongezeka mpaka kufikia pauni milioni 4.4.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad