Kikosi cha Yanga kipo mkoani Morogoro ambako kimeweka kambi ya muda mrefu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 23.
Yanga imeweka kambi Morogoro bila ya kocha mkuu Mwinyi Zahera ambaye yupo nyumbani kwake nchini Ufaransa baada ya kutolewa katika michuano ya Afcon ambapo anatarajia kuwasili baada ya muda mchache kumaliza mapumziko.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh amesema kuwa, Kocha Mwandila ameanza na mazoezi ya stamina ya kukijenga kikosi kabla ya kuanza mazoezi magumu ili kuhakikisha anawaweka
wachezaji sawa.
“Mazoezi anayoyatoa kocha kwa sasa ni yale ya stamina ya kujenga wachezaji kama inavyojulikana mazoezi ya mwanzoni mwa msimu, wachezaji wanafanya mazoezi asubuhi na jioni huku mwalimu akiwa anaendelea kukipanga kikosi ili kiweze kuwa imara.
“Baada ya kumaliza mazoezi hayo, ndio kocha atakapoendelea na mazoezi mengine kwa ajili ya kukiimarisha kikosi ambapo mwalimu akifika ataendelea pale atakapopakuta,” alisema Hafidh