Kutolewa Mapema Afcon ni Somo kwa Tanzania- Amunike

Kocha Mkuu wa Tanzania Emmanuel Amunike amesema michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika imekuwa ni funzo kubwa kwa Taifa Stars baada ya kutolewa mapema nchini Misri.

Tanzania, ambao imerejea kwa mara ya kwanza kwenye michuano hiyo baada ya miaka 39, imeshindwa kusonga mbele katika hatua ya mtoano baada kumaliza mkiani mwa kundi lao kwa kukubali kichapo kwenye mechi zote tatu walizocheza.

Kwa winga huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria na klabu ya Barcelona, hilo lilikuwa funzo kubwa ya kuwa ni namna gani mpira barani Afrika umebadilika na kuimarika.

"Ni somo kubwa kwa mpira wa Tanzania. Hatukuwahi kushiriki toka mwaka 1980, mambo mengi yametokea ndani ya miaka 39, na mpira umebadilika na unaendelea kubadilika," Amunike ameiambia BBC.

Nani kuvaana na nani 16 bora Afcon?
AFCON 2019: Bashiri ushindi wa timu yako
Uganda Cranes wasusia zoezi Misri, kulikoni?
"Kitu cha msingi ni kuendana na mabadiliko haya na kuimarika kama timu. Kuna mengi ya kujifunza.

"Shida yetu kubwa ilikuwa ni kutokuwa na uzoefu. Hatuna uzoefu wa kutosha sababu tumezoea kucheza mpira bila kuwa na shinikizo kubwa."

"Lakini tumeona katika michuano hii pale unapokuwa na mpira, basi wapinzania wanakuweka katika shinikizo kubwa."

Tanzania ilionesha dalili njema kwenye mchezo wao dhidi ya majirani Kenya, lakini ilishindwa kabisa kufurukuta dhidi ya Senegal na Algeria.

Amunike, ambaye alinyanyua Kombe la Dunia 2015 akiwa kocha wa timu ya vijana wa chini ya miaka 17 Nigeria, amesema Tanzania itabeba mafunzo yote waliyoyapata baada ya kurejea kwenye ulimwengo wa kandanda la ushindani.

Haki miliki ya pichaCAF/TWITTER
"Hatukuwa wenye kujiamini ama kutulia pale ambapo tulikuwa tunamiliki mpira."

"Katika kila safari, kuna mchakato wa kujifunza. Tutakaporejea (nyumbani) itatupasa tujitathmini kwa undani na kuona ni kwa namna gani tutaboresha mpira wetu.

"Ni dhahiri kuwa katika mpira wa kisasa, kama huna uwezo wa kushindana hutakuwa na nafasi ya kushinda - na hilo ndilo tulilokutana nalo."

Amunike ambaye alishinda taji la Mchezaji Bora wa Afrika mwaka 1994 pia anaamini kuwa kuna mustakabali mzuri kwa soka la Tanzania.

"Ninafurahishwa na wachezaji wangu, wote tulifanya kazi kubwa mpaka kufikia hapa, hatukualikwa tulishinda," amesisitiza.

"Kama tutaendelea na ari hii, na kuboresha katika yale tufanyayo naamini tutakuwa kama timu."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad