INTER Milan imethibitisha kuwa ipo kwenye harakati za kumsajili straika wa Manchester United, Romelu Lukaku. Kocha wa Inter Milan, Antonio Conte anamtaka Lukaku ili kuongeza nguvu kwenye fowadi yake.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Inter Milan, Piero Ausilio alikwenda London juzi na kukutana na Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward.
Conte anamtaka Lukaku ili azibe pengo la Mauro Icardi, ambaye anatarajiwa kuondoka katika timu hiyo. Inter inataka kumaliza dili hilo la Lukaku mapema baada ya kupata taarifa
kuwa Juventus na Napoli nazo zinamtaka straika huyo.
“Tulifanya kikao na Manchester United kujadili uwezekano wa kumsajili Lukaku,” alisema Ausilio katika mahojiano na televisheni ya Sky Sport Italia.
Inter Milan, hata hivyo, inataka kumsajili straika huyo kwa mkopo wa miaka mawili na baadaye kumnunua kwa pauni milioni 63 (Sh. bilioni 181).
Manchester United haitaki mpango huo bali inachotaka ni kuona Inter Milan inatoa pauni milioni 75 (Sh. bilioni 215) na kumbeba Lukaku.