Luteni ‘feki’ JWTZ adakwa
0
July 29, 2019
Jeshi la Polisi Mkoani Singida limemkamata mkazi mmoja wa jijini Arusha, Amieli Stephano (29), kwa tuhuma ya kujifanya Ofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye cheo cha luteni.
Mtuhumiwa huyo alipohojiwa na polisi, alikiri kuwa yeye ni mkulima na hajaajiriwa mahali popote.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike, alisema mtuhumiwa alikamatwa Julai 17, mwaka huu saa 6 mchana katika viwanja vya ofisi ya mkuu wa mkoa Bomani mjini hapa.
Alisema uchunguzi wa awali, unaonesha mtuhumiwa alikuwa maeneo ya Bomani kumwombea ndugu yake achaguliwe kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
“Kabla ya kuwasilisha ombi hilo, mtuhumiwa alijitambulisha kwa maofisa wa JWTZ, kuwa yeye ni ofisa wa jeshi hilo.
“Baada ya kujitambulisha alionesha kitambulisho chake chenye namba D. 0595 kikiwa na jina la P. 15705 A.S Marco.
“Pamoja na utambulisho huo, maofisa wa jeshi walimtilia shaka luteni huyo na kuamua kumkamata,” alisema Kamanda Njewike.
Alisema polisi kwa ushirikiano na maofisa hao, walifanya upekuzi ndani ya gari la mtuhumiwa aina ya Toyota Corola lenye namba za usajili T 289 AUF na kukuta vitu mbalimbali.
“Katika upekuzi, tulifanikiwa kukuta picha za paspoti saizi tatu za mtuhumiwa, sare za JWTZ zenye cheo cha luteni na mihuri minne ya shule mbalimbali.
“Mali zingine ni Sh 170,000 taslimu, cheti cha kuhitimu elimu ya sekondari kidato cha nne na cheti cha kuzaliwa cha Aloyce Zawadiel Solomoni,” alisema.
Kamanda Njewike alitaja vitu vingine, ni vivuli vya vyeti vya elimu ya sekondari, cheti cha diploma, cheti cha udereva na cheti cha elimu ya sekondari, mali ya Nelsoni John Ntandu,” alisema.
Kamanda Njewike alisema katika upekuzi uliofanyika chumba cha nyumba ya kulala wageni, Rock Side ya Majengo mjini Singida, walikamata Sh 500,000.
Alisema polisi, wanaendelea na upelelezi zaidi na baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani