Magufuli Ndiye Pekee wa Kuwajibu Kinana, Makamba
1
July 17, 2019
By Luqman Maloto
Makatibu wakuu wastaafu CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana, wamesajili kwa umma wa Watanzania malalamiko yao kuhusu maneno ya Cyprian Musiba, anayejipambanua kuwa mwanaharakati mtetezi wa Rais na Serikali ya awamu ya tano.
Kupitia waraka wao ambao umesambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Makamba na Kinana wanalalamika kuchafuliwa na Musiba, vilevile kujengewa chuki kwamba wao wanamhujumu Rais Magufuli.
Katika waraka huo, Makamba na Kinana wameonyesha kushangazwa na kauli za Musiba kuwa wao wanasuka njama za kumdhibiti Rais Magufuli ili asipitishwe na CCM kuwa mgombea urais kwa muhula wa pili.
Jambo lingine ambalo limewaumiza ni namna Musiba alivuka mpaka na kuwatuhumu viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuwa wanamhujumu Rais Magufuli. Wanasema hatua hiyo si nzuri kwa afya ya Muungano.
Musiba ni nani?
Musiba ni mwandishi wa habari. Ni kada wa CCM aliyefanya jitihada za kugombea ubunge Jimbo la Mwibara, Mara, lakini alishindwa katika kura za maoni.
Musiba anatajwa kumiliki magazeti ambayo yamekuwa yakilalamiwa na baadhi ya wanasiasa, wanaharakati na watu wengine wakiwamo wastaafu kwamba yanawachafua na kuwaita watu hatari na wanaokula njama za kumhujumu Rais Magufuli. Wanasiasa mbalimbali wa CCM na vyama vya upinzani ni waathirika wa mkumbo wa maandishi ya magazeti ya Musiba. Mara zote wamekuwa wakilalamika lakini ufumbuzi wa kudumu haujapatikana.
Orodha ni ndefu ya waliotajwa na magazeti hayo. Mbali na Makamba na Kinana, wamo wabunge, Zitto Kabwe, Hussein Bashe, Nape Nnauye, Freeman Mbowe, mfanyabiashara Rostam Aziz, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu na wengine.
Musiba pia hufanya mikutano na waandishi wa habari, na kutaja majina ya watu anaowaita ni hatari na wanaomhujumu Rais Magufuli.
Vilevile, Musiba ambaye hurekodi video na kuzisambaza, pia husema yenye kuandikwa na magazeti yake hahusiki nayo kwa sababu si mhariri. Hivi karibuni baadhi ya wabunge walilalamika bungeni kuhusu magazeti hayo kuwashambulia baadhi ya wabunge. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliwajibu kuwa anayeona amechafuliwa aende mahakamani.
Mara ya kwanza Kinana alipotajwa na Musiba kuwa anamhujumu Rais Magufuli, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, alimwita Musiba kumhoji alipopata hizo habari, lakini hakuna hatua za wazi zilizochukuliwa. Zaidi, Musiba aliendeleza wembe uleule.
Membe ndiye mwathirika pekee wa mashambulizi ya Musiba aliyesajili malalamiko yake mahakamani na kesi inaendelea. Makamba na Kinana katika waraka wao wanasema, wamekaa kimya kwa kudhani Musiba angechukuliwa hatua, lakini hilo halijafanyika. Pia wamesema majina yao hayawezi kusafishwa kwa fidia.
Rais Magufuli asaidie
Waraka wa Kinana na Makamba, ukurasa wa kwanza, aya ya tatu, wanasema kuwa tamko lao limefuatiwa na ushauri wa viongozi wa kidini, viongozi wakuu wastaafu wa CCM, waandishi wa habari, baadhi ya wana CCM na wananchi wengine kadhaa.
Tambua kuwa Kinana na Makamba ni vigogo ambao wameihudumia nchi tangu Serikali ya awamu ya kwanza. Inapofikia hatua ya kulalamika hadharani, maana yake hilo jambo limekuwa zito kulimaliza kimyakimya.
Baada ya hapo, chukua maneno kuwa wametoa tamko baada ya ushauri wa watu wa kada mbalimbali, wakiwamo “viongozi wakuu wastaafu wa CCM”. Kiongozi mkuu wa CCM ni mwenyekiti, ambaye kwa sasa ni Rais Magufuli.
Hivyo, viongozi wakuu wastaafu CCM ni wenyeviti wastaafu; Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete. Waliopo hai ni Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Swali; je, Mwinyi, Mkapa na Kikwete wameshiriki kuwashauri Kinana na Makamba kutoa tamko?
Ukurasa wa pili, aya mbili za mwisho, Makamba na Kinana wanashangazwa na namna Musiba anavyozungumza mambo ya hatari kwa nchi lakini hachukuliwi hatua. Wanasema anakingiwa kifua. Papo hapo wanahoji ni nani huyo anamkingia kifua?
Bila kumung’unya maneno, Kinana na Makamba wanasema wamepata jibu la wanaomtuma Musiba, kwamba ni watu wenye mamlaka makubwa, hivyo wanampa ulinzi na kumkingia kifua aweze kusema chochote bila kuhojiwa na yeyote.
Wanasema watu hao wanaomlinda, wanafanya hivyo kwa sababu maalumu na kwa ajili ya kuwashughulikia walengwa ili kuwahusisha na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini.Pamoja na kusema Musiba apuuzwe, Makamba na Kinana wanasema wamemwandikia barua Katibu wa Baraza la Ushauri la viongozi waastafu CCM, Pius Msekwa. Mwinyi ndiye mwenyekiti wa baraza hilo.
Kumbuka kuwa Makamba na Kinana wametangulia kusema waliomba ushauri kwa “viongozi wakuu wastaafu CCM” na kuwashauri watoe waraka. Halafu, Makamba na Kinana wamewaandikia barua ya malalamiko haohao viongozi wakuu wastaafu CCM. Kuna majibu tofauti yatapatikana?
Kwa mtazamo mwepesi ni kuwa kama viongozi hao wakuu wastaafu CCM wangekuwa na majibu tofauti, wangewaambia Makamba na Kinana, wasubiri washughulikie tatizo lao ndani kwa ndani. Kitendo cha kubariki watoe tamko hilo, kinaonesha jambo hilo ni gumu kwao. Hata hivyo, Msekwa amesema pia kuwa malalamiko hayo atayawasilishwa kwenye uongozi wa chama, ambacho kipo chini ya Rais Magufuli.
Kama suala hilo ni gumu kwa Makamba na Kinana na pengine kwa viongozi wakuu wastaafu, unaona kwamba hakuna mwingine wa kujibu huo, zaidi ya mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli.
Zaidi ya kuwa mwenyekiti CCM, vilevile ni mkuu wa nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Hakuna wa mtu wa kumkingia kifua mhusika, mwenye ubavu kuliko Rais Magufuli.
Mwananchi
Tags
Luqman Maloto. wewe ni mdau uliyevuka mpaka wako...!!!!
ReplyDeleteIna onesha wazi udhaifu ulio nao ikitawaaliwa na Chuki binafsi au unatumika .
Kumbuka wewena wallio kama wewe na fikira kama wewe.
Magu hajaribiwi . ana mambo enye umuhimu zaidi kwa maendeleo ya Taifa letu kuliko haya ya vijana wa zamani.
Uitakaa kujua haya mpigie mume wa Mama Anna Abdallah au nenda ferry ukaangalie Meli na upanuzi wa magati yetu.
kumbuka hapa ni kazi tu.
Na kaama huna unakaribishwa Ferry kushanga.
kwani wewe ni wa wapi??