Baada ya taarifa kueleza kuwa katika shambulio la kigaidi linalodhaniwa kuua watu 26 huko Kismayu Somalia, na miongoni mwa hao kuna mfanyabiashara Mahad Nur Gurguurte ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maisha Supermarket, uongozi umethibitisha.
Akiongea na EATV&EA Radio Digital, Meneja wa Maisha Supermarket Emodia Lloyd, amesema ni kweli Mahad Nur amefariki kwenye shambulio hilo.
''Alikuwepo kwenye hoteli ya Asasey ambayo imeshambuliwa, baada ya taarifa tulimtafuta hakuwa anapatikana kwenye simu, tukawasiliana na mtu mmoja huko akaenda kuangalia chumbani kwake hakumkuta ikabidi aende hospitali ndipo akakuta mwili wake'', ameeleza Emodia.
Emodia amesema kuwa kuna mtanzania mwingine ambaye aliambatana na Mahad Nur, kwenye safari hiyo ya kibiashara, yeye amejuruhiwa na yupo hospitali lakini bado hawajapata taarifa za maendeleo ya hali yake kwasasa.
Mahad Nur alikwenda Somalia siku 7 zilizopita na kufikia kwenye hoteli ya Asasey iliyopo mjini Kismayo ambayo ndiyo imeshambuliwa usiku wa kuamkia leo Julai 13, 2019.
Kuhusu taratibu za mazishi Emodia amefafanua kuwa msiba upo nyumbani kwa baba yake Kigamboni, lakini taratibu zinazoendelea huenda Mahad akazikwa leo huko Kismayo, kutokana na taarifa kueleza kuwa mwili umeharibika hivyo ni ngumu kuusafirisha.