Makombora ya Kirusi yawasili Uturuki licha ya vikwazo vya Marekani

Uturuki imepokea shehena ya kwanza ya makombora ya Kirusi ya S-400 licha ya upinzani mkali kutoka Marekani.

Shehena hiyo imepokelewa katika uwanja wa ndege wa jeshi leo Ijumaa kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara.

Hatua hiyo ya Uturuki kwa hakika itaikasirisha Marekani ambayo tarayi imeshaonya kuwa nchi hiyo haiwezi kumiliki zana za kijeshi za Urusi na Marekani kwa pamoja.

Makombora ya S-400 kutoka Urusi ni ya kujilinda na ndege vita, na wakati hu huo Uturuki imewekeza vilivyo katika ununuzi wa ndege vita aina ya F-35 kutoka Marekani.

Uturuki imeshasaini mkataba wa kununua ndege vita 100 aina ya F-35 kutoka Marekani.

Pia kampuni za Kituruki zinatengeneza takribani vipuri 937 vya aina hiyo ya ndege.

Uturuki na Marekani zote ni nchi wananchama wa Umoja wa Kujihami wa Nato, ambapo Urusi yaonekana ni adui mkuu wa umoja huo.

Hata hivyo, Uturuki imekuwa ikionekana kuwa na msimamo huru katika masuala ya ulinzi, kutokana na kuwa na uhusiano wa mashaka baina ya washirika wake wa Ulaya na Marekani.

Imenunua mfumo huo wa makombora ya S-400 kwa dola 2.5 bilioni, na kutuma maafisa wake nchini Urusi kwa mafunzo ya kutumia makombora hayo.

Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image caption
Marekani haitaki Uturuki imiliki makombora ya Kirusi ili kulinda ndege zake aina ya F 35
Hata hivyo, maafisa wa Marekani hawataki kabisa ndege zao aina ya F-35 kuwa karibu na makombora ya S-400 - wakihofia wataalamu wa kirusi wataweza kung'amua mapungufu ya ndege hizo.

Marekani imeenda mbali kwa kutishia kuitoa Uturuki kwenye mpango wa kuendeleza na manunuzi ya F-35 na kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.

Uturuki hata hivyo inasema mifumo hiyo ya Urusi na Marekani itawekwa kwenye maeneo tofauti.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema baada ya kukutana na rais wa Marekani Donald Trump kuwa haamini kama watawekewa vikwazo.

Lakini tayari Marekani imeshasitisha kutoa mafunzo kwa marubani wa Kituruki, na yaonekana kuwa jeshi la Marekani halina mzaha katika hilo.

Erdogan anacheza kamari kuwa Trump hana upinzani juu ya makombora hayo kama ilivyo kwa maafisa wa jeshi wa Pentagon.

Kwa hakika huu ni mwanzo wa mgogoro mpya wa kidiplomasia na ulinzi baina ya Ankara na Washington.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad