Malkia wa Afrika Chaka Chaka atua ZIFF

Malkia wa Muziki wa Afrika, Mama Yvonne Chaka Chaka tayari yupo visiwani hapa kwenye tamasha la 22 la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF)  ambapo atafanya shughuli mbalimbali ikiwemo makongamano na Wanawake pamoja na wadau wengine wakiwemo wasanii wa filamu na muziki.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Masoko wa ZIFF, Isihaka Mlawa amebainisha kuwa, Mama Yvonne ni miongoni mwa wageni maalum kwa mwaka huu ambapo pia atafanya shughuli za kijamii ikiwemo makongamano na warsha ya Wanawake, wasanii wa filamu na wale wa muziki shughuli zilizoandaliwa na ZIFF 2019.

“Mama Yvonne Chaka Chaka amefika jana Zanzibar na leo ataendelea na programu maalum ikiwemo kukutana na Wanafunzi wanaopata mafunzo ya filamu lakini pia atakutana na Wasanii wa muziki kutoka Chuo cha Muziki cha Dhow Country Music Academy.” Alieleza Isihaka.

Aidha, Isihaka Mlawa ameongeza kuwa, wanatarajia Mama Yvonne Chaka Chaka na mwanamuziki aliyeimba wimbo wa Zanzibar miaka 40 iliyopita, Sipho Mabuse kufanya tukio maalum la muziki kidogo kwenye shughuli za tamasha hilo linaloendelea visiwani hapa na kutarajiwa kufikia tamati Julai 14, mwaka huu.

Mama Yvonne Chaka Chaka na Sipho Mabuse wapo visiwani hapa kama wageni maalum waalikwa wa tamasha hilo kwa mwaka huu ambapo wamekuwa kioo na kielelezo kutokana na nyimbo zao mbalimbali zilizotamba Bara la Afrika pamoja na umaarufu wao katika jamii inayowazunguka.

Msanii Mama Yvonne Chaka Chaka (Jina la kuzaliwa Yvonne Machaka ambapo alizaliwa mnamo mwaka 1965 ni mwimbaji kutoka Afrika ya Kusini.

Kuitwa kwake Malkia wa Afrika ni kutokana na kuwa mstari wa mbele katika muziki maarufu wa Afrika Kusini kwa miaka 20.

Nyimbo kama "I'm burning Up", "I'm in Love with a DJ", "I Cry for Freedom", "Makoti", "Motherland" na "Umqombothi" ("Pombe ya Afrika") zimeweza kumuweka kwenye ramani ya Afrika na kuwa maarufu zaidi.

Msanii huyo alizaliwa Dobsonville huko Soweto na alikuja kuwa mototo wa kwanza wa Kiafrika kuonekana kwenye televisheni Afrika Kusini. Mwaka 1981 "Sugar Shack", kipindi cha wenye talanta, kilimjulisha kwa umma wa Afrika Kusini.

Katika harakati za muziki, Chaka Chaka alianza kuimba akiwa na miaka 19 mwaka 1985 wakati Phil Hollis wa Dephon Records alimgundua mjini Johannesburg- Muda mfupi baada ya albamu yake "I'm in Love With a DJ", kuuzwa nakala 35,000.

Pia katika nyimbo zake zilizowahi kushinda tuzo mbalimbali ni kama "Burning Up", "Sangoma", "Who's The Boss", "Motherland", "Be Proud to be African", "Thank You Mr DJ", "Back on my Feet ", " Rhythm of Life "," Who's got the Power "," Bombani (Tiko Rahini), "Power of Afrika", "Yvonne and Friends" na "Kwenzenjani".

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad