BAADHI ya wanazuoni wa Dini ya Kiislamu na Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum wamewaonya mashehe wanaomfanyia dua msanii Wema Sepetu kuwa wawe makini vinginevyo watamsababishia matatizo, Risasi Jumamosi lina habari kamili.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa njia na nyakati tofauti wanazuoni hao walisema misingi ya dua isipofuatwa huweza kumdhuru anayesomewa.
KWA NINI DUA IDHURU?
“Dua inapoombwa kwa mtu humfanyia wepesi jambo analoliombea; lakini dua ina mazingatio yake.
“Kwa sababu mashehe hutoa maneno kwenye Kitabu cha Kurani Tukufu ambacho kinakemea maovu, sasa kama mtu ataombewa kwa aya zilizopo ndani ya kitabu kitakatifu halafu yeye akaendelea kufanya maasi huonekana kama anamchezea Allah (Mungu).
“Mimi ushauri wangu, hao mashehe wasiishie kumuombea Wema na watu wengine bila kuwaongoza katika njia ya kuishi kwa kufuata mambo ya Mwenyezi Mungu,” alisema Maalim Othman Hamis Mkazi wa Manzese.
Naye Aboubakar Hassan ambaye ni Ustaadhi katika Msikiti wa Kichangani ulioko Magomeni, Dar alisema:
“Kuomba dua ni jambo zuri, lakini ni vibaya mtu kuombewa juu ya matatizo yaleyale kwa dua zilezile maana yake mtu huyo hataki kubadilika na kufuata njia njema.”
SHEHE ALHAD ANENA
Mwandishi wetu alipomuuliza kwa njia ya simu Shehe wa Mkoa wa Dar, Alhad kuhusu ukweli wa kauli za wasomi hao wa dini alisema, wametoa ushauri wa maana.
“Siyo kwa Wema tu kama mtu maarufu ni kwa watu wote, unapomshirikisha Mungu kwenye matatizo yako kwa kumuomba dua basi naye anakutarajia uzifuate njia zake.
“Ni hatari sana mtu kuombewa dua mara kwa mara kwa kosa lilelile kwa sababu maneno wanayotamka mashehe yanatoka kwenye Kurani Tukufu, usipokuwa makini unaweza badala ya kupunguza matatizo yako ukajikuta yameongezeka kwa sababu unaonekana kuchezea maneno ya Mungu,” alisema Shehe Alhad.
WEMA AAPA KUTULIA
Kufuatia kuandamwa na matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakimfikisha kwenye vyombo vya sheria mara kwa mara, Wema amesema katika mahojiano yake mara kadhaa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa, sasa anataka kuishi maisha yaliyo mbali na skendo.
Mmoja kati ya rafiki zake wa karibu na msanii huyo alimwambia mwandishi wetu hivi karibuni kuwa:
“Jamii inatakiwa kumtambua Wema kama mtu mpya kuanzia sasa.
“Wema kwa sasa anajitambua, anajua alipoteleza, amepevuka kiakili na yupo tayari kutimiza kusudi lililomleta duniani.
“Sote tunajua kuwa Wema ni kipenzi cha watu mwenye nguvu ya ushawishi na mtu muhimu kwenye jamii,” alisema rafiki huyo aliyejitaja kwa jina moja la Borry.
HITIMISHO
Hivi karibuni Wema alifutiwa dhamana na mahakama na kujikuta akipelekwa mahabusu kwenye Gereza la Segerea ambako alikaa kwa siku saba kabla ya kurejeshwa tena mahakamani na kudhaminiwa.
Wema anakabiliwa na shitaka la kupiga na kusambaza picha zisizokuwa na maadili kwenye mitandao ya kijamii na kwamba kesi yake bado inaendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar.