Leo July 16, 2019 Rais Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Butimba Mkoani Mwanza kusikiliza kero za Wafungwa.
Mmoja wa wafungwa anayetumikia kifungo cha miaka 30, Kalikenya Nyamboge, amemtuhumu Ofisa Usalama gerezani hapo kuwapa wafungwa simu halafu zikikamatwa wananyan’ganywa vitu vyao walivyo navyo lakini hadi leo hajafanywa kitu chochote.
“Mheshimiwa rais, huyu ofisa akupe mihuri na hizo simu uondoke nazo utajua mwenyewe utaenda kufanyia nini na ikibidi ondoka naye kwani ukifanya hivyo utakiwa umetusaidia sana na ukimuacha atanidhuru.
“Sasa hivi Jenerali Kamishna ametuletea daktari msomi na alivyofika vifo ndiyo vimepungua maana walikua wakikuchoma sindano wanakuua.
“Na si mara ya kwanza wao kuua mimi nilikuwa nimepanga nikitoka nije kukwambia na nikitoka nitakuletea mambo yote yanayotokea huku lakini huyu usimuache maana kwa Mwenyezi Mungu utakua umeandika maelezo ya mauji,” amesema Nyamboge.
Naye mfungwa mwingine Kulwa Alphonce, alikamatwa mwaka 2017 akiwa na mafuta ya dizeli akapelekwa Kituo cha Nyegezi askari wakamuomba Sh milioni moja, akawaambia ana 200,000 tu ambayo walikataa kisha baadaye wakampeleka ‘central’ baada ya hapo akafunguliwa kesi ya mauaji.
Aidha, mfungwa mwingine Shukrani Masegenya, alimuomba Rais Magufuli kuwapunguzia adhabu ya vifungo ili wakatumie ujuzi wao wanaofundishwa nje.
Akizungumza baada ya kuwasikiliza wafungwa na askari magereza , Rais Magufuli amesema kufika kwake gerezani hapo kuna somo kubwa limemuingia na akwenda kulifanyia kazi.
"Niliyoyasikia lazima nifanyie kazi, nimesikia changamoto za wafungwa na nimesikia pia changamoto za askari wangu.Niahidi nitayafanyia kazi yote ambayo nimeyasikia kwenu wote,"amesema Rais Magufuli na kuongeza hayuko tayari kuona askari magereza wanalalamika wakati yeye yupo.
Rais Magufuli amefafanua kwenye gereza hilo la Butimba amegudua mambo mengi , amebaini kuna kuombwa rushwa wafungwa na mahabusu na uamuzi wake wa kufika hapo umetokana na kufahamu mambo mengi ambayo mengine wafungwa wameshindwa kueleza.
Amewahakikishia wafungwa hao kwamba amewaelewa wafungwa na mahabusu hao na kuahidi kuwa amewasikia na yote ambayo ameleezwa yatafanyiwa kazi."Niahidi nimewasikia, nimewasikia na yote nitayafanyia kazi.Naomba muwe wavumilivu na niaminini."
Rais Magufuli amesema hata walioko uraiani ni wafungwa au mahabusu wabadae na kwamba kufungwa au kuwa mahabusu haina maana ya kukosa haki za kibinadamu.