Mkuchika "Tanzania Inazidi Kupata Heshima Katika Mapambano Dhidi Ya Rushwa"


Na Mwandishi Wetu, MAELEZO
WAZIRI wa nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), George Mkuchika amesema Tanzania inaendelea kupata heshima kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa katika vita vya mapambano dhidi ya rushwa kutokana na mshikamano na nguvu ya pamoja iliyopo katika vyombo na taasisi zinazosimamia utawala bora nchini.

Akizungumza katika kongamano la siku maalum dhidi ya rushwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam leo Jumatano (Julai 3, 2019) Waziri Mkuchika alisema utafiti uliofanywa na taasisi hizo zimesifu juhudi za zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na kuitaja Tanzania kuwa ni nchi ya mfano katika vita vya mapambano dhidi ya rushwa.

Mkuchika aliasema taasisi hizo zikiwemo MO Ibrahim, Transparency International, APRM na taasisi nyingine kubwa duniani zinazosimamia masuala ya utawala bora zimefanya utafiti na kusifu juhudi kubwa zinazofanywa na  serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. John Magufuli katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo tafiti mbalimbali zimeifanya Tanzania kushika nafasi ya pili nyuma ya nchi ya Rwanda.

Waziri Mkuchika alisema Serikali ya Awamu ya tano imeendelea kuweka mkazo na msukumo  katika mapambano dhidi ya rushwa ambapo taasisi zote zinazosimamia masuala ya utawala bora zimekuwa zikiunganisha nguvu ya pamoja na kulifanya suala la rushwa sasa kuwa na nguvu na msukumo mpya wa mapambano katika jamii.

“Kwa sasa vyombo vyetu vyote serikalini si TAKUKURU pekee bali pia polisi, tiss (usalama wa taifa), Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ICAG) na vingine vyote, vimeendelea kuunga katika kusimamia masuala ya utawala bora na hili limeleta msukumo na hamasa mpya katika vita dhidi ya rushwa hapa nchini” alisema Waziri Mkuchika

Akizungumzia rushwa katika sekta ya viwanda na biashara, Waziri Mkuchika alisema Serikali imeendelea kuweka mikakati mbalimbali katika kupunguza tatizo hilo ambalo limekuwa likiathiri sekta binafsi ambayo imekuwa mshirika wa karibu wa serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika alisema rushwa katika sekta biashara imekuwa ikiathiri sana masuala ya uwekezaji wa kigeni, ambapo eneo lililonyesha kutawala kwa rushwa ni katika eneo la utoaji wa vibali na leseni kutoka katika taasisi na idara muhimu za serikalini na hivyo serikali imeendelea kulifanyia kazi ili kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo vinaondolewa kwa wawekezaji na hivyo kuharakisha ukuaji wa uchumi.

Akifafanua zaidi Mkuchika anasema kutokana na serikali kutambua mchango wa sekta ya viwanda na biashara katika kukuza uchumi na uzalishaji wa ajira nchini ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali imekuwa ikifanya marekebisho mbalimbali ya sheria na sera mbalimbali ambazo zimekuwa ni sehemu ya mianya ya rushwa nchini ikiwemo eneo la kodi.

“Kutokana na kudhibiti rushwa kwa sasa kiwango cha ukusanyaji wa mapato ya mwezi yameweza kuongezeka kutoka Tsh Bilioni 800 kwa mwezi hadi kufikia Tsh trilioni 1.3 hii inaoyesha kuwa kulikuwa na maeneo ambayo kulikuwa na uvujaji wa mapato ya serikali kulikochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo rushwa”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Diwani Athumani alisema serikali imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kupitia Mpango Mkakati dhidi ya mapambano ya rushwa (NASCAP III) ili kuhakikisha kuwa mapambano na vita dhidi ya rushwa yanapata mafanikio nchini.

Anaongeza kuwa kupitia NASCAP III, ofisi yake imeendelea kutekeleza masuala mbalimbaliu ikiwemo kufanya tafiti kubaini ukubwa na kiwango cha rushwa nchini, kupokea maoni, kutoa elimu kwa umma kupitia makongamano, rushwa pamoja na kufanya uchunguzi na kufungua mashtaka kwa watu mbalimbali wanaopatikana na hatia dhidi ya rushwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad